Watoto 25 wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi wamefanyiwa upasuaji katika awamu ya kwanza ya kambi ya upasuaji inayoendelea Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI), iliyoratibiwa na MOI kwa ushirkiano na chama cha  wazazi  wenye watoto wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi Tanzania (ASBATH) chini ya ufadhili wa taasisi ya MO Dewji Foundation.

Daktari bingwa wa Mbobezi wa Ubongo, Mgongo na Mishipa ya Fahamu MOI Dkt. Hamisi Shabani amesema watoto hao ni kati ya 50 wanaotarajiwa kufanyiwa upasuaji katika kambi hiyo ya matatibu.

“Jumla ya watoto wote katika mpango huu ni 50, katika awamu hii ya kwanza ya upasuaji watoto 25 wamefanyiwa upasuaji na Mei, 4, 2024 watoto 25 waliobakia watafanyiwa upasuaji ili kukamilisha malengo ya kambi hii” amesema Dkt. Shabani ambaye pia ni mratibu wa kambi hiyo na kuongeza kuwa

“Watoto hawa wanafanyiwa upasuaji kwa kutumia teknolojia ya hali ya juu ya upasuaji wa kutumia matundu, ETV, upasuaji ambao humfanya mgonjwa kuruhusiwa kurudi nyumbani ndani ya siku chache tangu kufanyiwa upasuaji”

Amesema bado tatizo la vichwa vikubwa na mgongo wazi ni kubwa hapa nchini ambapo takwimu zinaonesha kuwa watoto 7500 wanazaliwa na tatizo hilo ila mwaka.

“Sisi MOI kwa mwaka jana tuliweza kuwafanyia upasuaji watoto wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi 800 hii inaonesha bado kuna wimbi kubwa la watoto ambao hawajapata matibabu”

Kwa upande wake Mratibu wa Miradi wa MO Dewji Foundation Amina Ramadhani amesema lengo la msaada huo ni kuwawezesha watoto hao kupata matibabu ili waweze kurejea katika hali zao za kawaida.

“Maisha ya kila mtu ni muhimu, iwapo kutakuwa na ongezeko la watoto zaidi ya 50 tutaangalia namna ya kuwasaidia ingawa lengo la mwaka huu lilikuwa watoto 50, tunawashukuru MOI na chama cha wazazi wenye watoto wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi (ASBATH)”

Merina Damon na Mohamed Hamisi ni wazazi wa watoto wenye vichwa vikubwa waliofanyiwa upasuaji wameishukuru MOI, chama cha wazazi wenye watoto wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi (ASBATH) MO Dewji Foundation kwa msaada wa matibabu hayo.







Share To:

Post A Comment: