Na Mwandishi wetu, Handeni.
WANANCHI waliohama kwa hiyari kutoka eneo la hifadhi ya Ngorongoro kwenda Kijiji cha Msomera wilayani Handeni mkoani Tanga wamemuomba mkuu wa mkoa huo mhe. Balozi Dkt.Batilda Salha Burian kumfikishia salaam za shukrani Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuwahamisha kwa hiyari kutoka ndani ya hifadhi hiyo na kuwajengea huduma bora za kijamii nje ya Hifadhi.
Wananchi hao wakiongozwa na makamu mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Ngorongoro mhe. Emmanuel Gabriel Tonge na madiwani waliohama kutoka Ngorongoro kuelekea katika Kijiji hicho wamesema kuwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan amewaondoa kwenye mateso ya muda mrefu ya kuishi na wanyama hatarishi, kutokuwa na uhuru wa kufanya shughuli za kiuchumi kutokana na kuzuiliwa na sheria za hifadhi pamoja na Watoto wao kushindwa kupata elimu bora walipokuwa Ngorongoro.
“Mhe. mkuu wa mkoa tunakuomba sana mfikishie salaam zetu Mhe. Rais wetu Dkt.Samia, huyu mama amejawa na utu, huruma na upendo kwetu sisi wananchi wa Ngorongoro, bila msimamo wake tungeendelea kuishi katika hali ngumu ndani ya hifadhi kwani changamoto ndogondogo zilizopo hapa Msomera hazilingani na ugumu wa maisha uliopo ndani ya hifadhi”alisema Mhe. Gabriel Tonge.
Madiwani waliopata nafasi ya kuzungumza katika kikao hicho wamesisitiza umuhimu wa wananchi waliopo Ngorongoro kujiandikisha kuhama kwa hiari ili waweze kutumia fursa lukuki zilizopo Msomera.
Katika ziara hiyo iliyokuwa na lengo la kutatua kero za wananchi kwenye Kijiji cha Msomera Dkt. Burian amesikiliza changamoto mbalimbali za wananchi ili Serikali iendelee kuzifanyia kazi kutimiza azma ya maisha bora ya wananchi katika Kijiji hicho.
Amesema serikali imetenga fedha za kutosha kupitia sekta za barabara, kilimo, umeme, mifugo, maji, mawasiliano, elimu na afya katika kuboresha huduma hizo kijijini hapo ili wananchi wengi waliopo ndani ya hifadhi ya Ngorongoro waweze kuhama kwa hiyari na kufaidi huduma hizo muhimu.
Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Handeni mhe. Albert Msando amesema serikali katika ngazi ya wilaya imeweka kambi kijijini hapo katika kuhakikisha kuwa kila changamoto inayoibuliwa na wananchi inapatiwa majibu ili kutekeleza maelekezo ya serikali ya awamu ya sita ya kuhakikisha kila mwananchi anakuwa na maisha bora kwa kutatua changamoto zao.
Post A Comment: