Na Imma Msumba : Ngorongoro
Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) imezindua zoezi la upigaji kura kuwania tuzo ya kivutio bora cha utalii barani Afrika kwa mwaka 2024 katika hafla iliyofanyika ukumbi wa Jengo la Ngorongoro Jijini Arusha.
Akizindua kampeni hiyo ya upigaji kura kaimu kamishna wa Uhifadhi NCAA Victoria Shayo amesema zoezi hilo litachukua siku 131 kuanzia mwezi huu wa aprili na linatarajiwa kukamilika mwezi Septemba 2024.
Amesema eneo la hifadhi ya Ngorongoro mwaka jana lilifanikiwa kushinda tuzo hiyo inayoandaliwa na mtandao wa World travel Awards baada ya kushinda katika kinyang’anyiro hicho kilichohusisha vivutio vingine vya Table Mountain, Harbeestpoort aerial cableway, V & A Waterfront, Ruben Island vya Afrika kusini, ziwa Malawi, Okavango Delta ya Botswana, Pyramids of Giza ya Misri pamoja na hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro hali iliyoitangaza nchi yetu na kuongeza idadi ya watalii.
Kamishna Shayo amesema tuzo hizo zina umuhimu mkubwa katika kuendeleza sekta ya utalii nchini na duniani kwa ujumla na kutoa wito kwa watanzania na wageni wote wanaotembelea Tanzania kuipiga kura nyingi Ngorongoro ili kuiwezesha Ngorongoro kutetea taji lake.
Akizungumzia kuhusu ongezeko la watalii nchini Kaimu Kamishna ameeleza kuwa mpaka kufikia nusu mwaka wa fedha wa 2023/24 hifadhi ya Ngorongoro imeshaingiza watalii zaidi ya laki saba ambapo wageni hao wameweza kuiwezesha mamlaka kupata zaidi ya shilingi bilioni 170.
Kwa upande wake Meneja wa Huduma za Utalii NCAA Mariam Kobelo ametoa wito kwa vyombo vya habari kuendelea kuwahamasisha wananchi kuhusiana na umuhimu wa kutembelea vivutio vya utalii na kupata elimu kuhusiana na vivutio hivyo.
Naye Afisa Utalii Mkuu wa NCAA Bw. Peter Makutian amewapongeza wageni wote waliotembela hifadhi ya Ngorongoro ambao kutokana na hamasa yao ya kupiga kura kwa wingi mwaka 2023 kuliiwezesha hifadhi ya Ngorongoro kuwa kivutio bora cha utalii barani Afrika kwa mwaka 2023.
Katika mwaka huu wa 2024 jumla ya Nchi tano barani Afrika za tuzo hiyo ambazo ni Tanzania, Afrika Kusini, Botswana, Misri na Malawi zinawania tuzo hiyo.
Post A Comment: