Na Happy Shayo
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) amekutana na kufanya mazungumzo na wadau wa uhifadhi, Frankfurt Zoological Society (FZS) kutoka Ujerumani na Six Rivers Africa (SRA) ya Tanzania ambao wamekuwa wakiisaidia Serikali katika maeneo mbalimbali ya uhifadhi ikiwemo urejeshaji wa wanyama waliotoweka (restoration),utafiti, kupambana na ujangili na kusaidia jamii kujikwamua kiuchumi hasa zinazoishi pembezoni mwa maeneo ya hifadhi pamoja na masuala ya utalii.
Kikao hicho kimefanyika leo Aprili 22,2024 katika ukumbi wa hoteli ya Gran Melia jijini Arusha.
Akizungumza katika kikao hicho, Mhe. Kairuki ameendelea kuwaomba ushirikiano katika uhifadhi ikiwemo ufuatiliaji wa idadi na kufanya sensa ya wanyamapori katika mifumo ikolojia mingine ambayo muda wa sensa ya wanyamapori umechelewa akitolea mfano wa ikolojia za Burigi-Chato, Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi, Malagarasi-Moyowosi-Kigosi na Serengeti.
Pia, amewaomba wadau hao kushiriki katika kujengea uwezo wahifadhi hasa kuhusu maendeleo ya teknolojia katika kufanya sensa ya wanyamapori na kununua vifaa vilivyoboreshwa vya ufuatiliaji wa wanyamapori na kutoa ufadhili katika tafiti za aina muhimu za Wanyamapori wakiwemo Faru, Tembo, Wanyama Wanyama Wakubwa (Simba, Chui, mbwa mwitu).
Katika hatua nyingine, amewaomba ushirikiano katika kuimarisha teknolojia kwenye kupunguza mwingiliano baina ya Binadamu na Wanyamapori ili kupunguza madhara yanayotokea kwa wananchi, kusaidia katika zoezi la urejeshaji wa shoroba za wanyamapori na kuimarisha teknolojia katika ufugaji nyuki katika maeneo yanayozunguka Hifadhi za Serengeti na Nyerere kwa ajili ya maisha ya jamii na kuboresha miundombinu (nyumba, doria barabara na viwanja vya ndege).
Post A Comment: