Na Damian Kunambi, Njombe


Wanachama na viongozi wa vyama vya ushirika (AMCOS) wilayani Ludewa mkoani Njombe wameiomba serikali kuwapa kipaumbele katika ununuzi wa mazao yao ili kuwezesha ukuaji wa uchumi wa vyama hivyo sambamba   na ongezeko la idadi ya wanachama watakao jiunga na vyama hivyo.

Wakizungumza mbele ya mkuu wa wilaya ya Ludewa Victoria mwanziva, Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, viongozi wa Chama cha mapinduzi pamoja na wakuu wa idara ya kilimo ngazi ya mkoa na wilaya katika kikao kazi na vyama vya ushirika wilaya ya Ludewa ambapo wanachama hao wamewasilisha changamoto mbalimbali zinazo wakwamisha katika ukuaji wao ikiwemo changamoto hiyo ya kutopewa kipaumbele cha ununuzi wa mazao yao.

Yohana Mhagama ni mwanachama wa AMCOS  kutoka kijiji cha Shaurimoyo kilichopo katika kata ya Lugarawa amesema wanaiomba serikali kupitia kitengo chake cha Hifadhi ya chakula NFRA pindi unapofika muda wa ununuzi wa mahindi vyama hivyo vipewe kipaumbele katika ununuzi wa mahindi.

" Tunaomba unapofika wakati wa uuzaji mazao ya mahindi kwenye utaratibu wa kununua mazao kupitia hifadhi ya chakula basi wavione vyama vya ushirika kuwa ndiyo jicho la kwanza ili kuleta chachu kwa wakulima kuona umuhimu wa kujiunga na vyama hivyo".

Naye Mwenyekiti wa AMCOS kata Luilo John Ngatunga ameeleza changamoto ya kushuka kwa kiwango cha uzalishaji wa  korosho kuwa ucheleweshaji wa viwatilifu ni kikwazo kikubwa kwao na kumepunguza kasi ya uzalishaji wa zao hilo.

"Nalia na nyinyi viongozi wa Wilaya naomba kujua tatizo ni nini? kuna changamoto nyingi lazima nizitaje hapa kwanza kuna ucheleweshwaji mkubwa wa viwatilifu na upatikanaji wa Sulphur". Amesema Ngatunga

Aidha kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Ludewa Victoria Mwanziva amesema lengo la kikao kazi hicho ni kutathmini mwelekeo wa vyama vya ushirika wilayani humo vilipotoka, vilipo na vinapoeleke ili kuhakikisha kuwa kunakuwa na kilimo chenye tija wilayani humo.

" Yote tuliyojadili leo ni kuhakikisha kuwa tunakuwa na kilimo chenye tija. Rais wetu Samia Suluhu Hassan ametupendelea Ludewa maafisa ugani wetu wote Wana pikipiki za kuweza kufika mashambani ili kuweza kutupa huduma za ugani, lakini tumepata vipima udongo ( soil scanner ) tunavyo,tunavitumia na tutaendelea kuvitumia.

Amesema amesikiliza changamoto zao na kuzipokea na wataendelea kuzifanyia kazi ili kuhakikisha wanakuwa na kilimo chenye tija na kupata matokeo chanya yatakayo pelekea mkulima mmoja mmoja kuinuka kiuchumi.

"Hatutaki kurudi nyuma, tunataka kusonga mbele tunataka kilimo chenye tija, chenye faida tunataka kuona wakulima wetu wakifaidika, wakinufaika". Amesema Mwanziva.

Hata hivyo  Mkurugenzi wa halmashauri hiyo Sunday Deogratius amesema wamezipokea changamoto hizo na kuahidi kuzifanyia kazi huku akieleza namna ambavyo wameweka mkakati katika kukuza uzalishaji wa zao la kahawa.

"Zao la kahawa ni moja ya mazao ya kimkakati katika halmashauri yetu, na tayari tumeanza kuchukua ujuzi kwa jirani zetu mkoa wa Mbeya ambao tuna uhakika utatuletea mabadiliko chanya katika kilimo chetu". Amesema Mkurugenzi. 

Akitolea ufafanuzi  ya changamoto Afisa kilimo wa wilaya hiyo Godfrey Mlelwa amesema kuhusu soko la mahindi wanunuzi wakubwa ni NFRA, lakini kwa upande wa vyama vya ushirika kumekuwa na changamoto kidogo lakini NFRA wanaangalia njia nzuri ya kuwawezesha vyama vya ushirika  kupeleka mazao yao huku Mrajisi wa vyama vya ushirika Mkoani Njombe Edmund Masawe akiwataka wanachama wa vyama hivyo kujisajili katika mfumo ili waweze kupata fursa mbalimbali

Share To:

Post A Comment: