Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) leo Machi 20, 2024 amekagua mabanda ya Maonesho yatakayotumika katika Maadhimisho ya Siku ya Misitu Duniani na Siku ya Upandaji Miti Kitaifa yanayotarajiwa kufanyika Machi 21 ambapo Mgeni Rasmi katika Kilele hicho anatarajiwa kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango.
Akitembelea mabanda yaliyopo kwenye Maonesho hayo, Mhe. Kairuki ameipongeza Wizara pamoja na Wadau wa misitu waliojitokeza kwa ajili ya kutoa elimu kuhusu majukumu yanayotekelezwa na taasisi zao ikiwemo elimu ya uhifadhi pamoja na kuonesha bidhaa mbalimbali zinazozalishwa na mazao ya misitu.
Mhe.Kairuki ametumia fursa hiyo kuwataka Wakazi wote wa Wilaya ya Same, Mkoani Kilimanjaro pamoja na Mikoa ya jirani kujitokeza kwa wingi kutembelea maonesho hayo.
Amesema maonesho hayo ni muhimu kwao kwani wataweza kujifunza masuala mbalimbali ikiwemo elimu ya ufugaji nyuki kibiashara pamoja na kujua fursa mbalimbali zinazopatikana katika mnyororo wa thamani ya mazao ya misitu.
Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Misitu Duniani na Siku ya Upandaji miti Kitaifa hufanyika kila mwaka Machi 21ambapo kwa mwaka huu Tanzania inaadhimisha Kilele hicho kwa kupanda miti pamoja na kutembelea maonesho ya bidhaa mbalimbali zitokanazo na misitu na nyuki.
Post A Comment: