Na John Walter-Babati
Watu watano waliokuwa katika gari la mizigo Scania lililokuwa limebeba magunia ya mahindi, lenye namba za usajili T 582 DRY wamenusurika kifo baada ya gari hilo kufeli breki na kuacha njia kisha kugonga nyumba mbovu iliyokuwa pembezoni mwa barabara.
Ajali hiyo imetokea leo Januari 4,2024 kijiji cha Sigino wilaya ya Babati mkoani Manyara ambapo gari hilo lilikodiwa na mfanyabiashara Marira Salum aliyekuwa anasafirisha magunia 136 ya mahindi kutoka Kijiji cha Endasaki wilayani Hanang’ kuelekea wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro.
Majeruhi wa ajali hiyo wanapatiwa matibabu katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Manyara.
Mkuu wa Usalama barabarani wilaya ya Babati James Makumu aliyefika katika eneo la tukio ametoa rai kwa madereva kuendelea kuzingatia kanuni za usalama barabarani pamoja na kufanya uchunguzi wa vyombo vyao mara kwa mara.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Sigino kati amesema eneo hilo kumekuwa na matukio mengi ya ajali kwa kuwa kuna mteremko na kona kali.
Post A Comment: