WANAWAKE Wafanyakazi wa Shirika la Mawasiliano Tanzania TTCL wameshauri kuendeleza jitihada zaidi na ubunifu katika kutimiza malengo na kuleta mabadiliko katika nchi.
Aidha wamehimizwa kutosubiri kuwezeshwa bali watumie fursa zilizopo kujiwezesha huku wakitanguliza kujiamini katika majukumu yao ili kuongeza tija katika maendeleo ya Taifa.
Ushauri huo umetolewa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) Bi. Zuhura Snare Muro alipokuwa akizungumza na wanawake hao ikiwa ni sehemu ya shamrashamra za kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani.
Bi. Zuhura amewataka wanawake hao kutosubiri kuwezeshwa bali watumie uwezo walionao kuongeza ubunifu na kufanya kazi kwa bidii.
” Asilimia tisini ya kile mwanamke unachoweza ni jitihada zako mwenyewe hizo nyingine zilizobakia ni kuongezewa nguvu tuu,” alisema na kuongeza kuwa wanawake ni kundi la watu walio jasiri katika kila jambo chambo la msingi ni kuondoa uoga katika kazi na majukumu wanayopewa.
Amesema wanawake wanapaswa kujitambua, kujiamini na kuongeza weledi.
Kwa upande wake,Mhandisi, Leticia Tinkas amewashauri wanawake hususani waliopo katika kada ya uhandisi kuongeza jitihada kwa kuwa wao ndiyo chachu ya ukuaji wa Tehama na maendeleo nchini.
” Tunawapa moyo wanawake mbalimbali walioko idara za uhandisi hata wanafunzi walioko shuleni waendelee na jitihada zaidi za kibunifu ili kutimiza malengo na kuleta mabadiliko katika nchi.
Mkurugenzi wa sheria, Bi. Anitha Moshi amehimiza wanawake kutambua Mawasiliano yao yako katika Hali gani kuanzia ngazi ya jamii na hata kwa wale wanoafanya nao kazi kwani mawasiliano ni chachu ya kukuza uchumi na kuleta maendeleo.
Amesema wanawake wa Shirika la Mawasiliano wanapaswa kuhakikisha wanaimarisha Mawasiliano katika sehemu za kazi hususani kwa wateja wao kwani ndio msingi wa ukuzaji wa uchumi.
Post A Comment: