Wananchi wa Kijiji cha Ruhembe, Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Mkoani Morogoro wameiahidi Kamati ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kuitunza miundombinu ya shule mpya ya sekondari Miwa iliyojengwa kupitia Mradi wa Kuboresha Elimu ya Sekondari (SEQUIP).
Akizungumza Februari 20, 2024 kwenye ziara ya Kamati hiyo kukagua ujenzi wa shule hiyo, Mwenyekiti wa Kijiji cha Ruhembe Abdallah Kambi amesema “Kiukweli kwa sasa wananchi hatuna adha tena ya shule ya sekondari katika hiki kijiji tunamshukuru sana Rais, Mhe. Samia Suluh Hassan kwa kuendelea kupambana kuwekeza miradi ya elimu.”
Amesema hapo awali watoto wa kijiji hicho walikuwa wanapata changamoto ya kuenda shule sababu ni mbali na makazi na jiografia ya kijiji hicho kimezungukwa na mashamba ya miwa maeneo mengi yanaonekana ni pori amesema njiani, kulikuwa kunatokea matukio mengi na hasa kwa watoto wa kike kufanyiwa vitendo vya kikatili.
Ameongezea kwa kusema watoto hao wa kike walikuwa wanashindwa kumaliza shule sababu ya changamoto zikiwemo za umbali wa shule waliokuwa wanaenda, kufanyiwa vitendo visivyofaa kama kubakwa, kupata mimba na mambo mengine ambayo yalikuwa ni changamoto kwa watoto hao wakike.
Naye, mkazi wa Kijiji hicho Fitina Nganywela amesema uwepo wa shule hiyo imewasaidia pia wao kama wazazi kuwa na imani na watoto wao sababu shule hiyo ipo karibu na maeneo ya makazi ambapo ni rahisi hata kwa mzazi kumfuatilia mtoto maendeleo yake shuleni na mwenendo mzima wa elimu.
“awali watoto walikuwa wanatembea kilomita 21 kuifuata shule ya kidogobasi lakini kwa sasa shule hii kuengwa hapa imesaidia” amesema Nganywela
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Mhe. Shaka Hamdu Shaka ameishukuru Kamati kuwa chombo cha wawakilishi kwa wananchi katika kuwasemea changamoto zao huku akiahidi kuendelea kushirikiana na wananchi hao katika uendeleza amani na maendeleo katika Halmashauri hiyo.
Shule hiyo ilipokea sh. milioni 528 kwa maelekezo ya kujenga shule mpya ya sekondari Miwa kupitia mradi wa Kuboresha Elimu ya Sekondari (SEQUIP).
Post A Comment: