Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Mohamed Mchengerwa amewaagiza Wakuu wa Mikoa yote nchini kusimamia kwa makini usambazaji wa sukari na kuwachukulia hatua wafanyabiashara wote wanaohujumu upatikanaji wake.
Akitoa agizo hilo leo Februari 21, 2024 Ofisi ndogo za Wizara zilizoko magogoni jijini Dar es salaam, Waziri Mchengerwa, amesema Serikali kupitia Tangazo la Serikali namba 40 lililotolewa mwezi Januari,2024 lilitoa bei elekezi na kuwataka viongozi wote wa Mikoa na Wilaya kusimamia bei elekezi iliyotolewa na Wizara ya Kilimo kwenye maeneo yao.
“Katika kukabiliana na upungufu wa Sukari Serikali kupitia Wizara ya Kilimo iliruhusu uagizaji wa sukari ambapo zaidi ya Tani 100,000 ziliingizwa nchini na utaratibu wa upatikanaji wa mawakala wa kusambaza sukari unaratibiwa kwenye Ofisi za Makatibu Tawala katika kila mkoa.”
“Hivyo majina ya mawakala walioruhusiwa na Serikali kupitia Wizara ya Kilimo kusambaza sukari katika kila mikoa yameshatumwa kwenye Ofisi za Wakuu wa Mikoa yote nchini chini ya usamamizi wa Makatibu Tawala hivyo jukumu kubwa limebakia kwa Wakuu wa Mikoa na Wilaya kuhakikisha mnasimamia usambazaji na uuzaji wa sukari kote nchini.”
“Hakikisheni mnashirikiana na Bodi ya Sukari iliyopo chini ya Wizara ya Kilimo kuwakamata Wafanyabiashara wote wanaokwenda kinyume na maelekezo ya Serikali na maelekezo ya Tangazo la Serikali na taratibu za Kijinai haswa zinazohusu masuala ya uhujumu uchumi zichukuliwe kwa mfanyabiashara yeyote anayekiuka misingi ya Taifa letu,” ameelezeka Mchengerwa
Amesema hatarajii kuona Mkuu wa Mkoa au Wilaya yeyote akishindwa kusikiliza kero za wananchi na kushindwa kutoa taarifa ya namna Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inavyoendelea kuchukua hatua mbalimbali za kukabiliana na changamoto zinazowakabili wananchi katika maeneo yao.
Post A Comment: