Madaktari bingwa wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) kwa kushirikiana na madaktari bingwa wabobezi kutoka Chuo Kikuu cha Colorado cha nchini Marekani wanatarajia kuwafanyia upasuaji wagonjwa Tisa wenye matatizo ya uvimbe kwenye Ubongo kwa njia ya kisasa ya kutoboa tundu ndogo bila ya kufungua fuvu katika kambi ya mafunzo ya wiki moja inayoendelea MOI jijini Dar es Salaam.
Mkutano huo wa tatu wa kimataifa wa mafunzo ya matibabu ya kisasa upasuaji wa uvimbe kwenye ubongo yanalenga kubadilishana uzoefu na kuwajengea uwezo madaktari bingwa wazawa, wauguzi wabobezi na wataalam wengine umefunguliwa leo Februari, 19, 2024 na na muwakilishi wa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Dkt. Lemeri Mchome.
“Mwaka 2017 tulianza upasuaji wa uvimbe vya chini ya ubongo(Pituitary tumors) bila kupasua fuvu kwa mara ya kwanza. Madaktari wa MOI baada ya mafunzo na mashirikiano hayo wameendelea na upasuaji huo mpaka sasa kwa ufanisi mkubwa…
Kwa sasa hapa MOI takribani wagonjwa 572 tunawafanyia upasuaji wa vivimbe kwenye ubongo na karibia asilimia nne ya wagonjwa hawa bado wanaenda nje ya nchi kupata matibabu kwa vivimbe vilivyo ndani kabisa ya ubongo ambapo upasuaji wa kawaida unaweza kuleta madhara zaidi.
Hivyo mafunzo haya yatasadia uanzishwaji wa huduma hii mpya ya upasuaji wa uvimbe ndani ya ubongo (Stereotactic procedures).
Amesema kuwa kwa kuanzisha huduma hizi tutaondoa usumbufu na ucheweleshaji kwa wagonjwa wahitaji lakini pia kuokoa fedha za serikali.
“Tayari tunao madktari bingwa bobevu 13 wa upasuaji wa ubongo na tunategemea wawili watajiunga nasi mwishoni mwa mwaka huu hivyo tuna madaktari wa kutosha kuendesha huduma hizi mpya…
Kwa niamba ya menejiment ya MOI na Mkurugenzi Mtendaji, niwashukuru sana wenzetu wa Chuo Kikuu cha Colorado kwa ushirikiano huu” amesema Dkt. Mchome
Mratibu wa mafunzo hayo, daktari bingwa Dkt. Nicephorus Rutabasibwa amesema katika kambi hiyo ya matibabu wagonjwa Tisa watafanyiwa upasuaji.
Daktari huyo ameelezea mkakati wa kuhakikisha upatikanaji wa huduma za kibobevu katika taasisi ya MOI na umuhimu wake kwa ujumla kwa nchi yetu na hata nje ya mipaka yetu kama utalii tiba
Kwa upande wake Prof. Ryan Ormond wa Chuo Kikuu cha Colorado amesema mkutano huo wa tatu wa kimataifa wa matibabu ya uvimbe katika ubongo ni muendelezo wa ushirikiano baina ya chuo hicho na MOI.
“Pamoja na mafunzo haya pia tumetoa msaada wa vifaa tiba na vitabu kwa ajili ya kurahisisha mafunzo kwa vitendo…tunaishukuru MOI kwa ushirikiano huu muhimu ambao unalenga kukuza tasnia ya matibabu ya uvimbe kwenye ubongo” amesema Prof. Ormond
Mwenyekiti wa matibabu ya Uvimbe kwenye Ubongo wa chuo kikuu cha Colorado Pro. Kevin Lillehei amebainisha kuwa ushrikiano huo utaiwezesha MOI kuwa kituo cha umahiri cha matibabu ya uvimbe kwenye ubongo katika ukanda wa Afrika.
Kwa upande wake Muuguzi Mbobezi wa MOI, Dorcas Magawa amesema kuwa kwa upande wao mafunzo hayo yatawasaidia kutoa huduma bora za uunguzi kwa wagonjwa wenye matatizo ya uvimbe katika ubongo.
Post A Comment: