MRADI wa HEET unakwenda kuboresha miundombinu ya majengo na vifaa vya kujifunzia katika Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam kulingana na maendeleo ya Sayansi na Teknolojia na kukidhi mahitaji kwa kuwafikia Wanafunzi wengi zaidi.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Februari 7,2024 Jijini Dar es Salaam, Katibu Tawala wa Wilaya ya Ubungo Bw. Hassan Mkwawa ambaye alimuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam katika Mkutano wa Wadau wa Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi uliofanyika Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam, amesema kuwa mradi huo unaenda kuboresha mazingira ya ufundishaji kuendana na mabadiliko ya Teknolojia ambapo katika sekta ya kilimo,biashara na ICT wanafunzi watanufaika.
“Kama tunavyotambua Sasa hivi Dunia ipo kwenye mabadiliko makubwa ya kiteknolojia, wanaita Artificial intelligence (Akili bandia) inaendana na mabadiliko ya vitu vingi, huwezi kuwa na matumizi ya akili bandia kama huna vifaa na watu wenye uwezo ambao wamefundishwa mambo yanayoendana na haya”. Amesema Bw. Mkwawa.
Aidha Bw. Mkwawa amesema mradi huo umekusudia kwenda sambamba na mabadiliko ya Teknolojia na uchumi wa ulimwengu kwa kuzalisha wanataaluma wenye weredi mkubwa na wanaostahili katika soko la ajira.
Kwa upande wake Naibu Makamu Mkuu wa Chuo-Mipango, Fedha na Utawala na Mratibu wa Mradi wa HEET, Profesa Bernadeta Killian amesema kuwa mradi huo umekusudia kutoa vipaumbele vya kijinsia kwa kuzingatia mahitaji ya wanafunzi na walimu wenye mahitaji maalumu.
“Mafunzo tunayotoa tunaangalia idadi kubwa ya wanawake na watu wenye mahitaji maalumu,lakini pia tumekwenda shule za Sekondari kutoa elimu kuhusu mambo ya jinsia na masuala ya usawa wa Kijinsia katika Sayansi, hesabu na fizikia”. Amesema Prof. Kilian
Pamoja na hayo amesema mradi huo unatoa fursa kwa wataaluma mbalimbali kushiriki katika kutoa mafunzo ili kuwafikia watu vizuri kwa kubadilishana utaalamu.
Mradi huo umeanza mwaka 2020 na utafika tamati mwaka 2025 ambapo unakwenda kuweka maboresho makubwa katika sekta ya Elimu ya Juu kwa kuzalisha wataalamu wenye weredi na wanaoendana na mabadiliko ya Sayansi na Teknolojia.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Ubungo Bw. Hassan Mkwawa, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam, Prof. William Anangisye na Naibu Makamu Mkuu wa Chuo-Mipango, Fedha na Utawala na Mratibu wa Mradi wa HEET, Profesa Bernadeta wakiwa kwenye picha ya pamoja na wadau mbalimbali wa Elimu katika Mkutano wa Wadau wa Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi uliofanyika leo Februari 7, 2024 katika Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam,
Katibu Tawala wa Wilaya ya Ubungo Bw. Hassan Mkwawa akizungumza katika Mkutano wa Wadau wa Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi uliofanyika leo Februari 7, 2024 katika Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam,
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam, Prof. William Anangisye akizungumza katika Mkutano wa Wadau wa Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi uliofanyika leo Februari 7, 2024 katika Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam,
Wadau mbalimbali wa Elimu wakiwa kwenye Mkutano wa Wadau wa Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi uliofanyika leo Februari 7, 2024 katika Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam,
Post A Comment: