Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini wameupongeza Mgodi wa North Mara kwa kutelekeza Dhana ya Uwajibikaji wa Kampuni kwa jamii inayozunguka mgodi (CSR) hususani katika miradi ya maendeleo ikiwemo Elimu, Afya na Maji mkoani humo.
Hayo yamebainishwa leo Februari 21,2024 na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Nishati na Madini, Mathayo David Mathayo mkoani Mara wakati wa ziara ya kutembelea Mgodi wa North mara kwa lengo la kuangalia miradi ya maendeleo na kupata taarifa ya maendeleo ya mgodi huo.
Akizungumza wakati akitoa taarifa ya majumuisho ya ziara kwa wajumbe wa Kamati na menejimenti ya Mgodi, mwenyekiti Mathayo ameupongeza mgodi huo kwa kuweza kuzingatia mpango wa CSR katika kutekeleza miradi ya maendeleo kwa sekta ya Elimu , Afya na Maji katika maeneo mbalimbali yanayozunguka mgodi.
Pia, Mwenyekiti ameupongeza mgodi kwa kutengeneza Bwawa kubwa la maji taka (TFS) ambalo linatumia mifumo mizuri ya kisasa katika kudhibiti utunzaji wa maji taka yanayotoka mgodini.
Naye , Naibu Waziri wa Madini Dkt.Steven Kiruswa ameutaka mgodi kufanya tafiti za madini katika maeneo mengine yaliyo karibu na mgodi na kuwapatia wachimbaji wadogo ili nao wajihusishe na uchimbaji ili kujenga uhusiano mzuri baina ya mgodi na wananchi wanaozunguka mgodi huo.
Akitoa taarifa ya maendeleo ya mgodi , Meneja Mkuu wa Mgodi wa huo Apolinary Lyambiko amesema kuwa mgodi umekuwa kinara katika ulipaji wa kodi na hadi sasa kiasi cha Tshs.3.25 trilioni zimelipwa kama kodi.
Lyambiko ameongeza kuwa asilimia 96 ya wafanyakazi wa mgodi ni watanzania, huku asilimia 86 ya manunuzi ndani ya mgodi zinakuwa kwa wafanyabiashara wadogo
Post A Comment: