Na Elizabeth Joseph

Waandishi wa Habari wanawake wameshauriwa kujifunza lugha za mataifa mbalimbali ili kuongeza wigo katika kazi zao ikiwa ni pamoja na kupata fursa za kutoka nje ya Tanzania.

Ushauri huo umetolewa na Mkurugenzi wa Kampuni ya Off We Go Safaris Ltd Bi, Genevieve Mollel wakati wa Uzinduzi wa Chama Cha Waandishi wa Habari Wanawake Mkoa wa Arusha(AWM) uliofanyika mkoani humo.

Amesema endapo Waandishi hao watajua lugha tofauti za mataifa mengine itawawezesha kupata fursa za kupata kazi kwa haraka hasa pindi wageni wanapokuja nchini kwa kazi mbalimbali ikiwemo Utalii.

"Waandishi mna nafasi kubwa ya kupata fursa kulingana na watu mnaofanya nao kazi kila mara hivyo mkijua lugha nyingi mfano Kijapan,wanapokuja nchini kufanya Utalii inakuwa rahisi kuchaguliwa ili kuongozana nao kuliko wao kuja na Waandishi wao,hii itafanyika hata kwa wageni wengine wakija nchini kwa shughuli nyingine"alifafanua Bi, Genevieve.

Naye Mwenyekiti wa Chama hiko Bi Jamila Omary amebainisha lengo la kuanzisha Chama hiko kuwa licha ya kuhabarisha jamii kupitia vyombo vyao vya habari lakini pia ni pamoja na kujikwamua kimaisha kwa kuwezeshana kupata miradi mbalimbali ya kujiingizia kipato.

"Chama hiki kitasaidia kupaza sauti zetu na kuleta mabadiliko kwenye maisha yetu,kazi zetu na jamii kwa ujumla hivyo kupitia Chama hiki tutumie fursa zinazotolewa mbali na Uandishi ili kujikwamua kimaisha mfano ipo mikopo inayotolewa na CRDB tunaweza kukopa na kuwezeshana ili kuanzisha miradi itakayo tusaidia kufanya miradi ya kujiongezea kipato "aliongeza Bi,Jamila.



Kwa upande wake Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Arusha Bw,Claud Gwandu licha ya kupongeza Uzinduzi wa Chama hiko pia aliwataka Waandishi Wanawake kuunganisha nguvu ili kwa pamoja kuweza kutatua changamoto zinazowakabili wao na jamii kwa ujumla 

"Dunia ya Leo bila kuunganisha nguvu hamuwezi kufanikisha hivyo niwaombe wanawake wengine kujiunga na Chama hiki ili kuwa na sauti ya pamoja "aliongeza kusema Bw, Gwandu.

Katika Uzinduzi huo mada mbalimbali zilitolewa ikiwemo Malezi na familia,Maadili ya Uandishi wa Habari pamoja Ujasiriamali na kuweka Akiba.



Share To:

Post A Comment: