Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), kupitia Chuo cha Ualimu wa Ufundi Stadi Morogoro (MVTTC), wametia saini hati ya makubaliano ya ushirikiano na Taasisi ya Karume ya Sayansi na Teknolojia (KIST) ya Zanzibar, lengo ni kuimarisha utoaji wa mafunzo ya ualimu wa ufundi na ufundi stadi ili kuzalishaji nguvu kazi yenye ujuzi mahiri sambamba na mabadiliko ya sera ya elimu na mitaala. Mabadiliko haya yanahusisha uanzishwaji wa mchepuo wa Mafunzo ya Amali kuanzia ngazi ya Sekondari, hivyo kusababisha mahitaji makubwa ya walimu wa mafunzo ya ufundi na ufundi stadi.
Makubaliano ya ushirikiano huo yamesainiwa leo, tarehe 21 Februari, 2024 visiwani Zanzibar, kati ya Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Dkt. Prosper Mgaya, na Mkuu wa KIST, Dkt. Mahmoud Abdulwahab Alawi, na kushuhudiwa na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Mhe. Lela Mohamed Mussa.
Kwa mujibu wa hati ya makubaliano, ushirikiano huo utajikita katika kubadilishana taarifa za uandaaji na utekelezaji wa mitaala ya ualimu wa ufundi na ufundi stadi; kuendesha programu za kubadilishana wakufunzi, vifaa vya kufundishia na nafasi za mazoezi kwa vitendo kwa wanafunzi; kufanya utafiti na kutoa huduma za ushauri elekezi, pamoja na uandishi na utekelezaji wa miradi yenye kuboresha utoaji wa Elimu na mafunzo ya Ufundi na Ufundi Stadi.
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Mhe. Bi. Lela Mohamed Mussa, amesema ushirikiano huo ni muhimu sana na utakuwa kichocheo katika kuwezesha utekelezaji wa Mabadiliko ya Sera ya Elimu (Majereo 2023) kuhusu Mafunzo ya Amali ambapo walimu mahiri wanatakiwa ili kutoa mafunzo hayo kwa ufanisi.
“Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imefanya jitihada za makusudi kufanya maandalizi ya kuwezesha utoaji wa elimu Amali, ikihusisha ujengaji wa miundombinu ya kisasa. Hata hivyo lengo hili haliwezi kufikiwa pasipo kuwa na waalimu wa kutosha na wenye sifa stahiki. Ninaamini ushirikiano kati ya MVTTC na KIST utakuwa na mchango mkubwa katika kuwezesha suala hili,”amesema.
Mhe. Bi. Lela Mussa ameagiza uongozi wa VETA na KIST kusimamia kwa karibu utekelezaji wa Mkataba huo ili kuhakikisha malengo yaliyowekwa yanatekelezwa kwa ufanisi na kwa wakati.
Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Dkt. Prosper Mgaya, amesema ushirikiano kati ya KIST na MVTTC utawezesha upatikanaji wa walimu wenye ujuzi na uwezo wa kufundisha Mafunzo ya Amali ili kupanua wigo wa upatikanaji wa walimu mahiri wa ufundi sambamba na ongezeko wa vyuo vya ufundi unaoendelea kote nchini.
Amesema “kwa sasa VETA ina vyuo 81 vinavyotoa mafunzo ya ufundi stadi. Kwa sasa Serikali inajenga vyuo vya mafunzo ya Ufundi stadi 65, lengo ni ifikapo mwaka 2025 kila Wilaya iwe na chuo cha mafunzo ya ufundi stadi. Ongezeko la vyuo hivi limeongeza mahitaji ya walimu wa ufundi stadi wenye sifa stahiki ili kuzalisha wahitimu wenye ujuzi na wenye uwezo wa kuajiriwa au kujiajiri”.
Aidha, Dkt. Mgaya amesema VETA na KIST watabadilishana uzoefu katika ufundishaji, na kwamba VETA inategemea kuwatumia walimu wa KIST kusaidia katika kufundisha mafunzo yanayohusiana uchumi wa bluu ikiwemo mafunzo ya kilimo cha mwani, kwa kuwa tayari wana uzoefu mkubwa kwenye maeneo hayo.
Naye Mkuu wa KIST, Dkt. Mahmoud Abdulwahab Alawi, amesema anaamini Chuo chake kitanufaika na ushirikiano huo, hasa kwa upande wa kuzalisha walimu bora wa kufundisha Mafunzo ya Amali visiwani Zanzibar kwa kuzingatia uzoefu na umahiri wa Chuo cha MVTTC.
Aidha, Mkuu wa Chuo cha MVTTC, Bw. Samwel A. Kaali, amesema Chuo chake kitahakikisha ushirikiano huo unazaa matunda na kuwa sehemu kubwa ya kufanikisha azma ya Serikali za Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Muungano wa Tanzania ya kutoa elimu bora ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mafunzo ya Amali (VTA) ya Zanzibar, Dkt. Bakari Silima, amesema makubaliano hayo yatawezesha kuimarisha umahiri wa walimu wa Mafunzo ya Amali na hatimaye kutoa mafunzo bora kwa wahitimu wa Mafunzo ya Amali.
Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Dkt. Prosper Mgaya akibadilishana hati za makubaliano ya ushirikiano na Mkuu wa Taasisi ya Karume ya Sayansi na Teknolojia (KIST) Zanzibar Dkt. Mahmoud Abdulwahab Alawi yaliyofanyika Zanzibar na kushuhudiwa naWaziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Mhe. Bi. Lela Mohamed Mussa (katakati)
Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Dkt. Prosper Mgaya na Mkuu wa Taasisi ya Karume ya Sayansi na Teknolojia (KIST) Zanzibar Dkt. Mahmoud Abdulwahab Alawi wakisaini hati ya Ushirikiano baina ya Taasisi hizo mbili yaliyofanyika Zanzibar .
Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Dkt. Prosper Mgaya na Mkuu wa Taasisi ya Karume ya Sayansi na Teknolojia (KIST) Zanzibar Dkt. Mahmoud Abdulwahab Alawi wakisaini hati ya Ushirikiano baina ya Taasisi hizo mbili yaliyofanyika Zanzibar .
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Mhe. Bi. Lela Mohamed Mussa akizungumza mara baada ya Kusaini Makubaliano kati ya VETA naTaasisi ya Karume ya Sayansi na Teknolojia (KIST) ya Zanzibar,Mjini Zanzibar
Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Dkt. Prosper Mgaya akizungumza mara baada kusaini mbakubaliano kati ya VETA naTaasisi ya Karume ya Sayansi na Teknolojia (KIST) ya Zanzibar,Mjini Zanzibar
Picha za pamoja za makundi mbalimbali mara baada ya kusaini Makubaliano kati ya VETA na KIST,
Post A Comment: