TASISI  ya Tanzania Health Promotion Support (THPS), kupitia Mradi wa Afya Hatua unaofadhiliwa na Mpango wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kukabiliana na UKIMWI, kupitia Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (CDC), leo Februari 15 wamekabidhi jengo lililokarabatiwa la kituo cha tiba na matunzo, samani na vifaa tiba mbalimbali vitakavosaidia kufanya uchunguzi wa saratani ya mlango wa kizazi kwa wanawake zaidi ya 485,000 mkoani Pwani walio katika umri wa kupata watoto na wapo katika hatari ya kupata saratani hiyo.
Hafla ya makabidhiano hayo ilifanyika katika zahanati ya Mwendapole iliyopo ndani ya Halmashauri ya Mji wa Kibaha na kusimamiwa na ndugu Rashid Mchatta, Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani na kuhudhuriwa na Mkurugenzi Mwandamizi wa Takwimu na Sayansi wa CDC Tanzania, Dk. Ann Buff na ujumbe wao.
” Kwa niaba ya Serikali, napenda kuishukuru Serikali ya Marekani kwa  msaada mkubwa wa kudhibiti janga la UKIMWI na kuokoa maisha ya watu tunaoendelea kupokea mkoani Pwani kupitia CDC,” alisema Mchatta.
“Napenda kuwahakikishia CDC na THPS kwamba uongozi wa mkoa wa Pwani, na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ujumla tunatambua na kuthamini sana mchango wenu katika mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI, tutaendelea kuwapatia ushirikiano unaohitajika,” alisema.
Kwa upande wake, Dk. Ann Buff, Mkurugenzi Mwandamizi wa Takwimu na Sayansi wa CDC Tanzania alisema ushirikiano baina ya Serikali na CDC utasaidia kupunguza kiwango cha saratani ya shingo ya kizazi nchini ambapo kwa sasa ni asilimia 3.1.
“Kuongezeka kwa ushirikiano katika utoaji wa huduma na kinga dhidi ya saratani ya mlango wa kizazi baina ya Serikali ya Marekani na Tanzania kutapunguza magonjwa na vifo vitokanavyo na saratani nchini Tanzania,” alisema Dk. Ann Buff.
 Vifaa vilivyo kabidhiwa ni pamoja na mashine tano za ‘thermocoagulation’ na sita za ‘cryotherapy’ ambazo zitagawiwa kwa zahanati kumi na moja ili kusaidia kuongeza kasi ya matibabu ya mabaka katika  kizazi yaliyogundulika katika hatua za awali za saratani ya shingo la kizazi ndani ya mkoa huo.
Pamoja na vifaa hivyo, THPS imekabidhi vishikwambi 125 ambavyo vitatumika katika vituo 85 vya kutolea huduma za afya mkoani humo ili kuboresha uhifadhi wa kumbukumbu na rufaa zinazotolewa kati ya vituo vya kutolea huduma za afya  na  jamii.
Kadhalika, THPS imeikabidhi serikali ya mkoa wa Pwani samani za ofisi zinazojumuisha viti na meza za kisasa za ofisi, kabati za kuhifadhia dawa, kabati zakuhifadhia mafaili na madawati yatakayotumiwa na wapokea huduma  wanaohudumiwa vituo vya afya.
Katika hotuba yake Dk  George Anatory ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa THPS alisema kuwa  THPS imejizatiti kuendelea kuunga mkono jitihada  za serikali katika kuhakikisha kuwa Watanzania wote wanapata huduma bora za afya na kuweza kuchangia kikamilifu katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi ya nchi.
  “Tunaamini jengo hili na vifaa tulivyokabidhi vitasaidia kuboresha ufanisi na kuhakikisha utoaji wa huduma bora jumuishi za kinga, tiba na matunzo ya VVU na upimaji na kinga dhidi ya saratani ya mlango wa kizazi zitakazo pelekea  kuokoa maisha ya wakazi wa  mkoa wa Pwani”,  alisema Dk. Mbatia.
Kuhusu THPS
Tanzania Health Promotion Support (THPS) ni asasi isiyo ya kiserikali iliyoanzishwa mwaka 2011, chini ya Sheria ya asasi zisizo za kiserikali nambari 24 ya 2002.
THPS inafanya kazi kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania kupitia Wizara za Afya za Tanzania Bara na Zanzibar; Wizara ya Jinsia, Vijana, Wazee na Makundi Maalum Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Kwa ufadhili wa Mpango wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Misaada ya UKIMWI kupitia Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa, THPS  inatekeleza afua mbalimbali za VVU/UKIMWI, Kifua kikuu, kuzuia ukatili wa kijinsia dhidi ya watoto huduma za afya ya uzazi, uzazi, watoto wachanga, watoto na vijana mifumo ya habari ya maabara na usimamizi wa afya, na UVIKO-19.
Kuhusu mradi wa CDC/PEPFAR Afya
Mradi huu unalenga kutoa huduma jumuishi katika vituo vya afya (Kigoma, Pwani, Shinyanga na Tanga) na katika jamii (Kigoma, Pwani na Tanga). Huduma hizi ni pamoja na matibabu na matunzo ya watu wanaoishi na VVU, huduma za kitabibu za tohara kwa wanaume katika mikoa ya Kigoma na Shinyanga na programu ya DREAMS kwa wasichana balehe na wanawake wadogo katika mkoa wa Shinyanga.

 

Share To:

Post A Comment: