Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC) kimetoa wanafunzi 349 waliohitimu mafunzo ya fani mbalimbali za uongezaji thamani wanafunzi hao wamepata fursa za ajira ikiwemo kujiajiri katika maeneo mbalimbali nchini.


Hayo yamesemwa leo Machi 20, 2024 katika ofisi za kituo hicho jijini Arusha na Kaimu Mratibu wa TGC, Jumanne Shimba katika kikao kazi na waandishi wa habari ambao wapo kwenye ziara ya kutembelea miradi ya kituo hicho.

"Vijana wengi ambao wamehitimu katika kituo hiki wamepata nafasi ya kuajiriwa na kujiajiri ikiwemo katika kampuni zinazofanya shughuli za uongezaji thamani kutokana na kuwa na ujuzi wa kiwango cha juu."

Amesema, idadi hiyo ya wahitimu ni tangu kituo hicho ambacho kina usajili rasmi wa Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET) kianze kutoa mafunzo mwaka 2015.

Shimba amesema, kituo hicho kinatoa mafunzo ya muda mfupi katika fani ya ukataji na ung’arishaji wa madini ya vito, fani ya usonara, fani ya uchongaji wa vinyago vya vito.

Pia, utambuzi wa madini ya vito na utengenezaji wa bidhaa za mapambo na urembo ili kuongeza tija katika sekta ya madini na kuwapa fursa za ajira Watanzania.

"Sisi tunachowafundisha ni pale madini yanapotoka mgodini kuanza kuyafanyia uchambuzi mpaka pale ambapo madini yanafikia kuwa bidhaa, baada ya kuyaongezea thamani madini hadi kwenda kumfikia mteja."

Aidha, Shimba amesema, katika mwaka wa fedha kituo kimeingizwa katika orodha ya wanufaika wa mikopo kutoka Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu.

“Kwa hiyo mwaka huu wanafunzi 11, wameweza kunufaika na mkopo huo, na tunatarajia wanafunzi wengi zaidi kuweza kunufaika.”

Malengo ya TGC ni kudumisha ubora, viwango, uadilifu na taaluma katika utoaji wa huduma zinazohusiana na madini ya vito ili kufikia viwango vinavyotakiwa katika soko la Kimataifa.

Ziara hii ya siku sita katika kituo cha TGC inawajumuhisha waandishi wa habari za mtandaoni kutoka vyombo mbalimbali kwa lengo la kujifunza shughuli zinazofanywa na kituo hicho.
Share To:

Post A Comment: