WAKALA wa Huduma za Misitu Tanzania(TFS)umesema katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Rais Dk.Samia Suluhu Hassan umefanikiwa katika mambo mengi yakiwemo ya kuimarisha sekta ya uhifadhi ,ujenzi wa miundombinu na kutoa ajira kwa askari na maofisa zaidi ya 500.
Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu miaka mitatu ya Rais Dk.Samia Suluhu Hassan, Kamishina wa Uhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania(TFS)Profesa Dos Santos Silayo amesema katika kipindi cha miaka mitatu ya Rais Dk.Samia Suluhu Hassan wanajivunia uongozi wake ambao unajali na kuthamini uhifadhi.
“Tunatoa shukrani na kumpongeza Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kwa kutimiza miaka mitatu na katika jambo ambalo sekta ya misitu tunajivunia katika uongozi wake ni kuwa na kiongozi wa juu anayejali na kuthamini uhifadhi.
“Anatoa msukumo wa moja kwa moja yeye binafsi kwenye hilo tunamshukuru sana Rais Dk.Samia kwani katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wake tumefanikiwa kuimarisha uhifadhi wa misitu na misitu yetu imeendelea kushamiri,”amesema.
Ameongeza kuwa TFS wameongeza wigo wa upandaji miti ya aina mbalimbali lakini katika kipindi hicho cha miaka mitatu yeye mwenyewe Rais Samia anavyozungumzia suala la uhifadhi na utalii amekuwa akitoa mchango wa moja kwa moja kuhamasisha jamii ile dhana na nia ya uhifadhi wa mazingira.
Amesema Rais Samia amekuwa akijali viumbe hai kwa kuwa yeye mwenyewe anajali na anatekeleza kwa vitendo jambo hilo, kwa hiyo wanamshukuru Rais.“Ametusidia sana maeneo ya utalii tumefanya vizuri.
“Ametuongezea nguvu katika kupata maofisa na askari wa kulinda misitu yetu tumeajiri takriban askari 500 katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Rais Samia.Tumeboresha miundombinu yetu kwa ajili ya kupata ofisi na makazi ya maofisa na askari wetu,”amesema Prof.Silayo.
Aidha amesema kwa kipindi cha miaka mitatu peke yake wamewekeza Sh.bilioni 31 ambazo zimesaidia kujenga ya ofisi 88 kote nchini ya ofisi lakini wamenunua magari na mitambo ya kutosha.
“Takriban Sh.bilioni 18 zimetumika katika kipindi cha miaka mitatu na tumepata magari kwani tunayo magari madogo 113, mitambo 17, boti 10 na pikikipiki 164 katika kipindi cha miaka mitatu.
“Kwa kweli ni uwekezaji mkubwa umefanyika ambao katika hali ya kawaida usingeweza kuwepo lakini Rais kwa maelekezo yake ya moja kwa moja au kwa marekebisho ya mifumo mbalimbali imetuwezesha kufikia mafanikio haya kama taasisi, hivyo tunamshukuru Rais Dk.Samia,”amesisitiza
Pia ameongeza katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Rais Samia, TFS imeongeza ushirikishaji wa wananchi katika uhifadhi na utunzaji wa misitu kwani wao ndio wanaona faida ya moja kwa moja ya uwepo wa misitu hiyo.
Amesisitiza katika kusimamia rasilimali za misitu changamoto kubwa inakuja pale ambapo kunakuwa hakuna ushirikishwaji wa wananchi ambao ndio wasimamizi wa awali , hivyo TFS wameongeza nguvu katika kushirikisha wananchi
“Tunawashirikisha kwa kuwapa elimu kupitia vipindi vya kutoa elimu kwa umma katika televisheni , pia tunawapa elimu kuhusu umuhimu wa uhifadhi wa misitu na katika kuwavutia tumekuwa na miradi mbalimbali kwa wananchi kwa lengo la kutia hamasa.
“Kumekuwa na miradi kama ufugaji nyuki, lakini wengine ukuzaji wa miche ambapo tunawasaidia miche, hivyo wanakuza miche na kuuza katika maeneo yao.Pia tunawasaidia katika ujenzi wa madarasa , ofisi za walimu maabara na mabweni.
“Tumekuwa tukisaidia sekta ya afya kwa kuboresha miundombinu ukiwemo wa ujenzi wa zahanati kwa mfano kule kijiji cha Wachawaseme tumejenga hospitali yenye thamani ya Sh.milioni 274.Tunagawa miti kwa wananchi ambayo thamani yake ni takriban Sh.bilioni sita kwa mwaka ambayo tunawapa bure wananchi,”amesema.
Ameongeza wamekuwa wakiwashirikisha wananchi kwa kuwapa mbinu za kupambana na majanga katika maeneo ya misitu kwani kuna misitu yao ambayo inapata majanga ya moto, hivyo tunawashirikisha wananchi namna ya kupambana na majanga hayo.
Post A Comment: