Ujumbe wa Tanzania Februari 27, 2024 ulikutana na Uongozi wa Shirikisho la Wafanyabiashara wa Vito na Bidhaa za Usonara nchini Thailand (TGJTA) katika kikao kilichojadili kwa kina masuala mbalimbali yanayohusu biashara na maendeleo ya sekta hiyo kwa pande zote.
Akizungumza katika kikao hicho, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Madini Msafiri Mbibo alilieleza shirikisho hilo kuhusu dhumuni la ujumbe wa Tanzania kuwepo nchini humo na kusema ni pamoja na kushiriki katika Maonesho ya 69 ya Kimataifa ya Madini ya Vito na Usonara, kuendelea kujifunza kuhusu uendeshaji wa minada ya madini ya vito na kujifunza kuhusu shughuli za uongezaji thamani madini ya vito na biashara ya vito.
Kwa upande wake, Rais wa Shirikisho hilo Bw. Somchai Phornchindarak aliuelezea ujumbe wa Tanzania kuhusu sababu mbalimbali zilizopelekea nchi ya Thailand kuwa kitovu cha biashara ya vito na bidhaa za usonara duniani ikiwemo kufanikiwa katika sekta hiyo na kusema siri ni uwepo wa viwango vidogo vya kodi kwenye biashara ya vito na bidhaa za usonara jambo ambalo husaidia kuzuia utoroshaji, kuvutia biashara dhidi ya nchi nyingine na kuongeza mauzo nje ya nchi na hivyo kupelekea kuongeza upatikanaji wa fedha za kigeni na mchango kwenye Pato la Taifa.
Pia, Somchai aliongeza kuwa, nchi ya Thailand imeruhusu msamaha wa kodi ya forodha na kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kwa madini ya vito na bidhaa za usonara zinazoingia (import) na kutoka (export) nchini Thailand na kueleza kwamba, uzoefu duniani unaonesha kuwa biashara zenye mitaji mikubwa ya uwekezaji huwekewa viwango vidogo vya kodi, ikiwemo biashara ya vito na bidhaa za usonara ili kuvuta walaji na kusisitiza kuhusu ushirikiano wa pamoja kati ya Serikali na Sekta binafsi katika kuendeleza sekta hiyo.
Kufuatia hali hiyo, aliishauri Serikali ya Tanzania kufikiria kuhusu namna bora inayoweza kufanya ili kuendeleza sekta na biashara ya vito na kuongeza kwamba, inayo nafasi kubwa ya kuwa kitovu cha madini ya vito Afrika na duniani kutokana na rasilimali ilizonazo, mazingira ya uwekezaji na biashara, pia, uzoefu katika masuala mbalimbali ambayo imeendelea kujifunza kutoka Thailand na nchi nyingine.
Katika hatua nyingine, Shirikisho hilo limepongeza hatua ya Tanzania kupanga kurejesha minada ya vito na Maonesho ya Kimataifa ya Madini ya Vito ya Arusha na kueleza ni mwanzo mzuri wa kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha biashara ya Madini Afrika, kuiwezesha Tanzania kunufaika vilivyo na madini hayo na kuongeza kwamba shirikisho hilo litaendelea kuimarisha uhusiano wake na Tanzania ambao umekuwepo kwa kipindi kirefu.
Aidha, shirikisho hilo limeshukuru kwa mwaliko wa Tanzania unaolenga kuwakutanisha na wafanyabiashara wa Tanzania ili kuendelea kubadilishana uzoefu katika eneo hilo.
Mbali na ujumbe wa Wizara, pia Mbunge wa Jimbo la Ulanga, Mhe. Salim Hasham ambaye pia ni mfanyabiashara wa Madini ya vito alishiriki katika kikao hicho. Aidha, baada ya kikao hicho, ujumbe wa Tanzania ulipata nafasi ya kutembelea ofisi yake iliyopo Bangkok- Thailand ambapo Naibu Katibu Mkuu Mbibo alimpongeza mfanyabiashara huyo kutokana na juhudi zake anazozifanya na kuwataka watanzania na wafanyabishara kuiga na kujifunza kutoka kwake.
Post A Comment: