Waziri wa Madini Anthony Mavunde amesema serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imedhamiria kuwasaidia wachimbaji wadogo kupata taarifa sahihi za maeneo yao ili kuwaondolea changamoto ya kuchimba kwa kubahatisha.
Hayo yamesemwa leo na Waziri Mavunde katika Kijiji cha Utimbe,Kata ya Lupaso,Wilaya ya Masasi-Mkoa wa Mtwara wakati wa uzinduzi wa zoezi la eneo la majaribio la Utafiti wa kina wa miamba yenye viashiria vya madini (High Resolution Airborne Geophysical Survey) linalofanywa na Kampuni ya TUKUTECH LTD kwa ushirikiano na Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini (GST).
“Wachimbaji wengi wadogo wamepoteza mitaji na nguvu nyingi kwa kukosa taarifa sahihi katika maeneo wanayochimba.
Kupitia Vision2030 tutalifikia eneo kubwa zaidi la nchi yetu kwa kufanya utafiti wa awali wa viashiria vya miamba yenye madini ili kuwaongoza kwa usahihi wachimbaji wa Tanzania.
Mh Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amenunua mitambo 15 ya uchorongaji ambayo itawahudumia wachimbaji nchi nzima baada ya kuwa tumepata taarifa za awali za viashiria miamba madini”Alisema Mavunde
Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Jiolojia na Utafiti Madini (GST) Dkt. Mussa Budeba amesema taasisi yake imejipanga vyema kutekeleza zoezi la utafiti wa kina wa madini kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kwa lengo la kufikia kufanya utafiti wa kina kwa 50% kwa eneo la Tanzania ifikapo mwaka 2030.
Akitoa maelekezo ya awali Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya TUKUTECH LTD Mhandisi Tukupala Mussa Mwalyolo amesema kampuni yake ipo tayari kushirikiana na serikali katika kutimiza lengo la utafiti wa kina wa madini nchini ili kuchochea ukuaji wa sekta ya madini na kwamba wapo tayari kufanya kazi na wachimbaji wadogo nchini ili kuwapatia taarifa sahihi za maeneo yao.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Masasi ambaye pia ni mkuu wa Wilaya ya Nanyumbu Dkt. Stephen Mwakajumilo na Mbunge wa Jimbo la Lulindi Issa Mchungahela wameipongeza Wizara ya Madini kwa mkakati wa utafiti wa kina katika eneo la Masasi kwa kuwa litasaidia kuongezeka kwa shughuli za kiuchumi,ajira na kuchochea maendeleo katika wilaya hiyo.
Post A Comment: