Tamasha la utalii Wilayani Same Mkoani Kilimanjaro lililopewa jina la SAME UTALII FESTIVAL linatarajiwa kuzinduliwa na Waziri mwenye dhamana ya maliasili na utalii Nchini Angellah Kairuki.
Akizungumza na vyombo vya habari mapema hivi leo Mkuu wa Wilaya hiyo ya Same Mkoani Kilimanjaro Kaslida Mgeni amethibitisha kuwa uzinduzi huo utafanyika kwenye viwanja vya stendi ya mabasi mjini Same tarehe 23/02/2024 siku ya pili ya tamasha hilo ambalo linatarajiwa kuanza tarehe 22/02/2024.
Kaslida amesema kuelekea kwenye tamasha hilo maandalizi yamekamiika kwa asilimia kubwa kwani kila kitu Kiko vizuri na wanasubiria swala la muda tu.
“Tunatarajia kuwa mheshimiwa Waziri mwenye dhamana ya maliasili na utalii Nchini Angellah Kairuki kwenye uzinduzi wa tamasha letu la utalii Wilayani Same tarehe 23/02/2024 ikiwa ni siku ya pili ya tamasha letu kwani tunaanza rasmi zoezi letu tarehe 22/02/2024 kwakutembelea mabanda mbalimbali ya maonyesho ya bidhaa mbalimbali za wananchi wa Same ambao wanavitu vingi sana vya asili na watapata nafasi ya kutangaza bidhaa zao kupitia tamasha hili”.
“Lakini sambamba na hilo pia tutafanya utalii kwenye mlima kidenge siku ya tarehe 22/02 na tarehe 23/02 tutafanya utalii kwenye hifadhi ya Taifa ya Mkomazi na tarehe 24/02/2024 tutafunga tamasha letu kwa kupanda mlima shengena mahali ulipo msitu wa Chome utalii wa maeneo yote hayo umepangiliwa vizuri na kiingilio chake ni nafuu mno ili kila mtanzania aweze kufurahia vivutio vya utalii ndani ya Wilaya yetu “.
“Alisema DC Kaslida Same “.
Naye Mkuu wa hifadhi ya Taifa ya Mkomazi Wilayani Same Emmanuel Moirana amesema miongoni mwa vitu ambavyo vitawafurahisha watanzania na wageni Kutoka nje ya Nchi wakiwa ndani ya hifadhi ya Taifa ya Mkomazi kwenye tamasha hilo ni uwepo wa utalii wa Faru weusi ambao wamekuwa kivutio kikubwa kwa watalii wengi wanaoingia ndani ya hifadhi hiyo.
Moirana amesema pamoja na utalii huo wa Faru pia vipo vivutio vingine vingi ndani ya hifadhi hiyo kitu ambacho kitazidi kuongeza hamasa kubwa kwa watalii watakaofika kwenye tamasha hilo na kuingia ndani ya hifadhi hiyo.
Amesema toka kuanza kwa mchakato wa tamasha hilo kumekuwepo na ongezeko kubwa la watalii wa ndani ndani ya hifadhi hiyo na watalii hao wameendelea kujivunia hazina ya vivutio mbalimbali vya utalii ndani ya hifadhi hiyo.
Tamasha la Same utalii festival litafanyika kuanzia tarehe 22-24/02/2024 katika viwanja vya stendi ya mabasi mjini Same likiwa na lengo la kutangaza vivutio mbalimbali vya utalii Wilayani Same.
Post A Comment: