Na. WAF – Mbeya


Serikali kupitia Wizara ya Afya imepongezwa kwa juhudi kubwa  inayoendelea kufanya za kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi, mama na mtoto ikiwa ni kipaumbele cha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. 

Pongezi hizo zimetolewa leo Januari 18, 2024 na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe. Juma Homera wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha kujadili mikakati ya kupunguza vifo vinavyotokana na uzazi, mama na mtoto.

“Vifo vitokanavyo na uzazi, mama na mtoto vimeendelea kupungua nchini, pongezi kwa Wizara ya Afya kwa kuunga mkono juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan kwa vitendo.” Amesema Mhe. Homera

Amesema, Rais Dkt. Samia amefanya kazi kubwa ya kutafuta fedha za ujenzi wa jengo la kuhudumia mama na mtoto katika Hospitali ya Kanda ya Mbeya (META) na ununuzi wa vifaa vya kisasa.

“Kwa uwekezaji huu unaofanywa na Serikali ya Rais Samia ni lazima watumishi kuwa waadilifu na wazalendo kwa kufanya kazi kwa kuzingatia maadili ya kazi, Taaluma na weledi.“ Amesema Mhe. Homera

Aidha, Mhe. Homera amesema ili kunaondokana na changamoto ya upatikanaji wa damu salama ni lazima kuwe na mikakati ya pamoja kwa Mikoa ya nyanda za juu Kusini Magharibi kwa kuchangia damu salama.

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Dkt. Elizabeth Nyema amewataka watumishi wa Sekta ya Afya kuwajibika na kuzidisha ushirikiano ili kwa pamoja kuendelea kupunguza vifo visivyo vya lazima vinavyotokana na Uzazi, mama na mtoto. 

Kikao hicho chenye kauli mbiu ya ‘Uongozi na uwajibikaji ni chachu ya punguza vifo vitokanavyo na Uzazi, mama na mtoto’ kimehusisha watumishi kutoka Sekta ya Afya wa kanda ya nyanda za juu Kusini Magharibi kutoka Mkoa mwenyeji wa Mbeya, Songwe na Rukwa.

Share To:

Post A Comment: