1000684072


 Na Carlos Claudio , Dodoma.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika kumbukizi ya miaka 40 ya Hayati Edward Moringe Sokoine aliyekuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

 

Hayo yameelezwa na msemaji wa familia ya hayati Edward Sokoine, Bw. Lembris Kipuyo alipokutana na kuzungumza na waandishi wa habari leo Machi 28, 2024 jijini Dodoma, kwa lengo la kuwaalika watanzania wote kwenye ibada maalum ya kumbukizi ya miaka 40 ya Hayati Edward Moringe Sokoine.

 

Amesema ibada hiyo iliyoandaliwa na familia ikishirikiana na Taasisi ya Hayati Edward Moringe Sokoine itafanyika siku ya Ijumaa Aprili 12, 2024, saa 3:00 asubuhi katika Kijiji cha Enguik, Monduli Juu mkoani Arusha.

 

Ibada hiyo ya kumbukumbu ya Hayati Sokoine itawashirikisha viongozi mbalimbali wa serikali wakiongozwa na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan,” amesema Bw. Kipuyo.

 

Amesema lengo kubwa la kuanzishwa kwa Taasisi ya Hayati Edward Moringe Sokoine ni kuenzi mema aliyoyafanya kwani aliacha alama kubwa ambayo taifa linamkumbuka hadi leo na kueleza kuwa taasisi hiyo imejikita katika masuala ya elimu, kilimo, hifadhi ya mazingira, vyanzo vya maji pamoja na afya.

 

Bw. Kipuyo amesema,“Hayati Sokoine alikuwa mzalendo wa kweli, alipenda taifa lake na wananchi wake, alihakikisha kwamba rasilimali za nchi zinatumika na watanzania wote, aliwatumikia wananchi bila kubagua na alikuwa na hofu ya Mungu katika kufanya kazi zake.”

 

Hayati Sokoine alikuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika vipindi viwili wakati wa uongozi wa awamu ya kwanza.

 

Hayati Sokoine alizaliwa Agosti 01, 1934, kijijini Enguik, Monduli Juu wilayani Monduli, mkoani Arusha na kufariki Aprili 12, 1984 kwa ajari ya gari katika kata ya Dakawa wilayani Mvomero mkoani Morogoro akitokea bungeni jijini Dodoma.


4baf199d-8920-4e0a-85f3-a263545ab0f3
Share To:

Post A Comment: