Mbunge wa Jimbo la Kavuu na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe, Geophrey Pinda amekutana na watumishi wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kampasi ya Mizengo Pinda kwa lengo la kujua changamoto zinazokikabili chuo hicho.
Mhe, Pinda amekutana na watumishi hao sambamba na kupata nao chakula cha jioni tarehe 27 Februari 2024 nyumbani kwake Kibaoni katika halmashauri ya Mpimbwe wilayani Mlele mkoa wa Katavi.
Kikao hicho ni muendelezo wa juhudi za Mbunge huyo wa Jimbo la Kavuu kukutana na makundi mbalimbali ndani ya jimbo lake kwa lengo la kupokea changamoto na kero na baadaye kuizitafutia ufumbuzi.
Akizungumza katika kikao hicho, Mhe, Pinda aliwaambia watumishi hao wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kuwa, lengo la kufanya mazungumzo pamoja na kupata chakula cha jioni ni kutaka kufahamu changamoto zinazokikabili chuo hicho sambamba na kubadilishana mawazo.
Kwa mujibu wa Mhe, Pinda Chuo hicho Kikuu cha Sokoine cha Kilimo ni chuo nyeti na umuhimu kwa watanzania husan wale wananchi wa jimbo lake la Kavuu.
‘’Chuo hiki ni muhimu sana hususan katika jimbo langu la Kavuu kwa kuwa kinatoa mafunzo ya fani ambazo zinaweza kuwasaidia vijana wetu katika masuala ya nyuki, mazao pamoja uwindaji wa kitalii ’’ alisema Mhe, Pinda.
Aidha, Mbunge huyo wa Jimbo la Kavuu aliwaeleza watumishi hao wa SUA Kampasi ya Mizengo Pinda kukitumia vyema Kituo cha Redio Jamii cha Mpimbwe kilichozinduliwa hivi karibuni na Waziri Mkuu Mhe, Kassim Majaliwa Majaliwa kujitangaza ili wananchi wafahamu kozi zinazotolewa chuoni hapo.
‘’Tumeanzisha redio ya Mpimbwe katika halmashauri yetu hivyo ni vyema mkaitumia redio hii kujitangaza ili muweze kupata wanafunzi wengi’’ alisema Mhe, Pinda.
Watumishi wa SUA Kampasi ya Mizengo Pinda walimshukuru Mhe, Pinda kwa kuwaalika na kukutana nao nyumbani kwake ili kuwasilisha changamoto sambamba na kupata chakula cha jioni.
Wamebainisha kuwa, utaratibu huo utamsaidia sana mbunge wa jimbo hilo kujua changamoto za chuo na kuzitafutia ufumbuzi ambapo wameshauri utaratibu huo uwe endelevu.
Mbali na Mambo mengine watumishi hao wameonesha kutofurahishwa na mwamko mdogo wa wenyeji wa maeneo ya Mpimbwe kujiunga na chuo hicho cha SUA ambapo walimuahidi Mbunge kufanya uhamasishaji ili vijana wengi wajiunge ikiwemo kutumia redio ya Mpimbwe kujitangaza.
Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Kampasi ya Mizengo Pinda kilichopo katika halmashauri ya Mpimbwe mkoa wa Katavi kinatoa kozi tatu za Shahada ya Sayansi ya Usimamizi wa Rasilimali Nyuki, Stashahada ya Uzalishaji na Usimamizi wa Mazao pamoja na Astashahada ya Uongozaji Watalii na Uwindaji wa Kitalii.
Post A Comment: