Na Munir Shemweta, WANMM MPIMBWE
Mbunge wa Jimbo la Kavuu katika halmashauri ya Mpimbwe wilaya ya Mlele mkoa wa Katavi na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geofrey Pinda amekabidhi magari mawili ya wagonjwa kwa halmashauri ya Mpimbwe iliyopo wilaya ya Mlele mkoa wa Katavi ili kusaidia kusafirisha wagonjwa.
Hafla ya kukabidhi magari hayo imefanyika tarehe 3 Februari 2024 katika kituo cha Afya Isevya kilichopo halmashauri ya Mpimbwe wilaya ya Mlele na kuhudhuriwa na viongozi wa halmashauri hiyo wakiwemo madiwani.
Akizungumza wakati wa kukabidhi magari hayo Mhe. Pinda alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuliwezesha jimbo lake katika huduma za sekta ya afya ikiwemo ujenzi wa vituo vya afya na zahanati.
‘’Nimshukuru Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kusaidia ujenzi wa vituo vya katika jimbo langu, kwa kweli Mhe. Rais ameifanya Mpimbwe istawi’’ alisema Mhe. Pinda.
Ameitaka halmashauri ya Mpimbwe na Kituo cha Afya cha Isevya kuhakikisha magari aliyoyakabidhi yanatunzwa vizuri sambamba na kutumika kwa yale malengo yaliyokusudiwa ya kuwahudumia wananchi wa Mpimbwe.
Kwa mujibu wa Mbunge huyo wa jimbo la Kavuu, wakati anaingia madarakani mwaka 2020, vituo vya afya kwenye jimbo lake vilikuwa viwili na kuvitaja kuwa ni kile cha Usevya na Mamba.
Hata hivyo, ameweka wazi kuwa, kwa sasa katika jimbo lake vimeanzishwa vituo vingine vitatu vya Majimoto, Kibaoni, Kasansa Pamoja na Zahanati ya Mwamapuli inayokwenda kuanza kazi.
Amesema, ataendelea na juhudi mbalimbali za kuimarisha huduma za sekta ya afya katika jimbo la Kavuu kwa kuwa afya ni muhimu huku akiwaahidi wananchi wa jimbo lake kupambana kwa hali na mali ili jimbo hilo libadilike kimaendeleo na pale atakapomaliza muda wake aache alama itakayomfanya aendelee kukumbukwa.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mpimbwe Shamimu Mwariko amesema, jukumu la halmashauri yake ni kuhakikisha magari waliyokabidhiwa yanaenda kusaidia na kuboresha huduma za afya kwa wananchi wa Mpimbwe.
‘’Tutayalinda na kuhakikisha muda wote yanafanya kazi iliyokusudiwa ya kusaidia na kuboresha huduma kwa wananchi’’ alisema Shamimu.
‘’Nimshukuru Rais kwa kuhakikisha huduma zote za afya nchini ikiwemo Mpimbwe zinakaa vizuri na katika mwaka huu wa fedha halmashauri yetu inaenda kukamilisha vituo vyetu vya afya vitatu vya Majimoto, Kasansa na kibaoni kwa asilimia mia moja’’ Alisema.
Mhe. Pinda alikuwa jimboni kwake kwa ziara ya siku moja ambapo mbali na hafla ya kukabidhi magari ya wagonjwa aliwatembelea na kuwafariji wananchi wa jimbo lake waliopatwa na ugonjwa wa kipiundupindu katika eneo la Mwamapuli.
Post A Comment: