KAMPUNI ya Ombeni Logistics inayojihusisha na Usafirishaji, Uuzaji wa Vipuli vya magari na Huduma za Nyumba na Majengo imeratibu mafunzo maalumu ya kilimo na ujasiriamali ikiwa ni sehemu kuwajengea uwezo na kurudisha kwa jamii kwa wananchi wa Kata mbalimbali Wilayani Mwanga Mkoani Kilimanjaro.
Mafunzo hayo yalikuwa na lengo la kuwajengea uwezo katika kufanya kilimo chenye tija pamoja na kukabiliana ushindani wa biashara ya kilimo Wilayani humo.
Akizungumza mara baada ya mafunzo hayo mtaalam na mwezeshaji wa mafunzo hayo kutoka TAHA Abdon Joseph amesema, lengo la mafunzo hayo ni kujenga uelewa kwa wakulima juu ya namna bora ya kufanya kilimo chenye manufaa hususani katika zao la parachichi.
“Ili kupata mazao bora lazima kilimo kifuate hatua na taratibu na mkulima aweze kupata mazao bora na kipato…tumeeleza hatua kwa hatua kuanzia uandaaji wa mashamba, uchaguzi wa mbegu kulingana na mazingira, utunzaji wake na kuchanganya mazao pamoja na elimu ya ujasiriamali katika zao la parachichi.” Amesema.
Amesema, mafunzo hayo yamezingatia taratibu zote za kimazingira ikijumuisha hali ya hewa na kuwataka wakulima hao kuzingatia yaliyoainishwa katika mafunzo ili kupata tija katika kilimo.
Kwa upande wake Muasisi wa Kampuni ya Ombeni Logistics Bw. Said Sultan Mndeme amewashukuru wananchi hao kwa mwitikio mkubwa katika mafunzo hayo na kuahidi kuendelea kushirikiana nao katika kuinua sekta ya kilimo pamoja na kutatua changamoto mbalimbali kwa lengo la kuleta maendeleo Wilayani humo.
Pia Afisa Tarafa Usangi, Misonge Geofrey ameeleza kuwa mafunzo hayo yametoa maarifa kwa wakulima ambao hufanya kilimo kwa mazoea na kueleza kuwa elimu hiyo imefufua maarifa ya kitaaluma yatakayoleta tija katika uzalishaji.
Akizungumza kwa furaha mara baada ya kupata mafunzo hayo Sheikh wa Wilaya ya Mwanga Shwaib Msofe amesema elimu hiyo itawasaidia katika kufanya kilimo cha kisasa.
“Ukweli ni kuwa tulisubiri kwa shauku kubwa mafunzo haya na yamekuwa na manufaa makubwa kwetu na tunachoweza kuahidi ni kuwa tunakwenda kufanyia kazi yale yote tuliyofundishwa, hata hivyo tumefurahi pia kupatiwa miche ya zao la parachichi kwa ajili ya kwenda kupanda na tunaishukuru sana kampuni ya Ombeni kwa kutambua umuhimu wa sekta ya kilimo kwa sisi wakulima wadogo.” Amesema.
Mafunzo hayo yaliratibiwa na Ombeni Logistics kwa kushirikiana na TAHA, Maua Mazuri na East Est Seeds na Agricentric.
Mtaalam wa kilimo kutoka TAHA Abdon Joseph akitoa mada kwa wananchi wa Mwanga juu ya kilimo cha kisasa na Ujasiriamali na kuwataka wakulima hao kuzingatia yaliyoainishwa katika mafunzo hayo kupata tija katika kilimo.
Baadhi ya washiriki wakichangia mada wakati wa mafunzo hayo.
Mafunzo yakiendelea
Post A Comment: