NAIBU Waziri Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mhe. Deogratius Ndejembi amewaelekeza Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini kuhakikisha wanafunzi wote wenye sifa za kuandikishwa kwa darasa la kwanza na kujiunga kidato cha kwanza wanasajiliwa ndani ya muda uliopangwa.

Mhe.Ndejembi ametoa agizo hilo leo wakati alipotembelea na kukagua maendeleo ya zoezi la kuripoti kwa wanafunzi katika Shule ya Sekondari Kilolambwani iliyopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Lindi mkoani Lindi.

“Mwisho wa zoezi la kuripoti kwa wanafunzi wa kidato cha kwanza na uandikishaji wa darasa la kwanza ni Machi 31. Agizo langu kwa Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini ni kuhakikisha kuwa kila mwanafunzi mwenye sifa anapata nafasi ya kujiunga na masomo.”

“Niwatake pia watendaji wa ngazi za chini kuanzia mtendaji wa kijiji/mtaa, mtendaji wa kata na tarafa wote wanakua mstari wa mbele kuhakikisha wanashirikiana na walimu wakuu wa shule za msingi ambao wanafunzi wao wamefaulu ili kuwabaini ambao wazazi wao watazuia watoto wao kutojiunga na masomo,” amesema Mhe. Ndejembi.

Ametoa wito kwa wazazi nchini kutowanyima watoto wao haki ya msingi ya kupata elimu na kuwataka watendaji wa serikali kuwafichua kwa vyombo vya dola wazazi ambao wataruhusu watoto wao kwenda kufanya kazi za ndani na kuacha shule.

“ Serikali inayoongozwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan imefanya uwekezaji mkubwa sana kwenye sekta ya elimu. Shule hii ya Kilolambwani imegharimu Sh Milioni 570 hivyo wazazi msiwazuie watoto majumbani waacheni wakapate elimu ambayo ni bure haina malipo,” smesema Mhe Ndejembi.

Naye, Mbunge wa Jimbo la Mchinga, Mhe. Salma Kikwete ameishukuru Serikali kazi kubwa ya maendeleo inayofanywa kwenye jimbo hilo ikiwamo ujenzi wa Sekondari hiyo ambayo amesema imekuwa mwarobaini kwa wanafunzi ambao awali walikua wakitembea umbali mrefu.

&&&

Share To:

Post A Comment: