Chuo Kikuu Mzumbe kupitia Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi, “Higher Education for Economic Transformation – HEET Project,” Januari 8, 2024 kimekabidhi eneo la ujenzi wa Ndaki ya Tanga kwa Mshauri mwelekezi kwa Kampuni ya Mekon Arch. Consult Limited ya Dar es Salaam kwa ajili ya kuanza usanifu wa miundombinu.
Hafla hiyo imefanyika katika Wilaya ya Mkinga, Kata ya Gombero, kijiji cha Pangarawe Mkoani Tanga na kushuhudiwa na Mkuu wa Wilaya ya Mkinga Kanali Maulid Surumbu ambaye alimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Waziri Kindamba.
Awali akizungumza na wananchi wa Kitongoji hicho cha Pangarawe Kanali Surumbu amesema ni wazi kuwa ongezeko la miundombinu ya vyuo vikuu ni kukuza sekta ya elimu na kusaidia maendeleo katika nyanja ya Sayansi na Teknolojia.
Amesema ni muda muafaka kwa wananchi wa Tanga hususan wakazi wa Wilaya ya Mkinga kuchangamkia fursa zitakazotoka na utekelezaji wa mradi huo.
“Licha ya kwamba lengo la msingi ni kutoa elimu, ujenzi huu utatoa ajira na fursa za kimaendeleo. Hivyo sisi wakazi wa Wilaya ya Mkinga ni vema tukachangamkia fursa hiyo na kuwa walinzi wa mradi huu”. Amesisitiza Kanali Surumbu.
Naye, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Prof. William Mwegoha, amesema miundombinu itakayojengwa katika eneo hilo ni pamoja na Jengo la Taaluma, Hosteli mbili, Bwalo la Chakula, Jengo la Zahanati, mfumo wa majitaka, na tenki la maji lenye ujazo wa lita laki nne.
“Katika mradi huu mkubwa Serikali imetenga kiasi cha Dola za Kimarekani milioni 21 kwa ajili ya uboreshaji wa miundombinu katika Chuo Kikuu Mzumbe. Kati ya fedha hizi kiasi cha Dola za Kimarekani milioni 7 zitatumika kwenye ujenzi wa miundombinu ya Kampasi ya Tanga.” Amesema Prof. William Mwegoha
Amesema mradi utakapokamilika Chuo Kikuu Mzumbe kitaanzisha program mbalimbali za Sayansi na Sayansi Tumizi kama vile Uhandisi, Teknolojia na TEHAMA, usimamizi wa mifumo na katika hatua za awali program nyingi zaidi zitazidi kuongezwa kadiri ya mahitaji.
Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma, Utafiti na Ushauri, Prof. Eliza Mwakasangula amefafanua hatua za maendeleo ya mradi tangu ulivyoanza na kuelezea malengo yake na kuishukuru jamii ya Pangarawe kwa uongozi imara na ushirikiano na moyo wa kujitolea wakati wote wa utekelezaji wa mradi.
“Tunajivunia kuwa sehemu ya juhudi hizi za kuleta mageuzi katika elimu na tunaahidi kufanya kazi kwa bidii ili kuhakikisha mafanikio ya mradi huu kwa maendeleo ya elimu nchini Tanzania” Amesisitiza Prof. Mwakasangula.
Kwa upande wake Mhe. Danstan Kitandula Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii na Mbunge wa Jimbo la Mkinga amesema atahakikisha miundombinu wezeshi ikiwa ni pamoja na Barabara, Umeme na Maji vinafika katika eneo la Mradi ili shughuli zikamilike kwa wakati.
Nae Mshauri Elekezi kutoka Kampuni ya Mekon Arch. Consult Limited amewahakikishia wana Mkinga, kukamilika kwa michoro ya eneo hilo ndani ya miezi mitatu hadi minne.
“Niwahakikishie baada ya miezi mitatu hadi minne Mkandarasi atakuwa amewasili eneo husika na kuanza ujenzi utaanza.
Badala ya kuwa ndoto kwenye vitabu, sasa ni halisia, wanamkinga mtafaidi, majengo yatakayokidhi viwango vya ubora” Amesisitiza Dkt. Moses Mkonyi Mshauri Elekezi – Mekon Arch. Consult Limited.
Post A Comment: