Mahakama Kuu ya Tanzania, Kituo cha Usuluhishi imetoa Tuzo kwa Msuluhishi wa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA), Mhe. Safina Msuwakollo, katika hafla iliyofanyika katika ukumbi wa Julius Nyerere International Convention Centre (JNICC), jijini Dar es Salaam, Januari 16, 2024.
Mheshimiwa Safina ametunukiwa tuzo hiyo kutoka Kituo cha Usuluhishi Mahakama Kuu ya Tanzania, ikiwa ni sehemu ya kutambua mchango wake katika kuipatia suluhu migogoro mingi kwa mwaka 2023.
Aidha, Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, amesema ipo faida kubwa katika kumaliza migogoro katika hatua ya usuluhishi kwani inachangia katika kupunguza mlundikano wa madai na usuluhishi unasaidia kukuza uchumi pamoja na ushirikiano.
Naye Jaji Mfawidhi, Kituo cha Usuluhishi Mahakama Kuu Tanzania, Mhe. Zahra Maruma, amesema, Kituo cha Usuluhishi Mahakama Kuu kimefanya uchunguzi wa migogoro mbalimbali ikiwa ni katika kuhakikisha wanatafuta namna bora ya kutambua changamoto na kuzipatia ufumbuzi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi, Mhe. Usekelege Mpulla akizungumza baada ya hafla hiyo, amesema tuzo hii itakua chachu ya mafanikio katika kusuluhisha migogoro mbalimbali ya kikazi kwa lengo la kukuza uwekezaji na uchumi wa nchi. Aidha, Mhe. Mpulla ametoa wito kwa waajiri na waajiriwa kuweza kumaliza migogoro yao katika hatua ya usuluhishi ili kuweza kuokoa muda ili kuendelea na shughuli za uzalishaji hatimaye kukuza uchumi.
Ameongeza kuwa, Tume imejipanga kikamilifu kuhakikisha inatoa huduma bora kwa wananchi ikiwa ni pamoja na kuwafikia popote walipo na kuhakikisha migogoro inaisha kwa njia ya usuluhishi na haki kwa kila mmoja.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kupokea tuzo, Mhe. Safina Msuwakollo amesema migogoro inapoisha katika hatua ya usuluhishi inaboresha mahusiano, na kuongeza muda wa uzalishaji kwani wadaawa watapata muda wa kuendelea kufanya kazi.
Post A Comment: