NAIBU Waziri Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mhe Deogratius Ndejembi amesema Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kupitia mradi wa uboreshaji wa barabara za vijijini kwa ushirikishaji na ufunguaji wa fursa za kijamii na kiuchumi (RISE) ipo kwenye hatua ya usanifu wa barabara kiwango cha lami km 50 za awali katika Halmashauri ya Wilaya ya Handeni mkoani Tanga.
Mhe Ndejembi ameyasema hayo katika Kata ya Kabuku wilayani Handeni akiwa kwenye ziara ya Makamu wa Rais Dkt Philip Isdor Mpango.
“ Mhe Makamu wa Rais tunamshukuru sana Mhe Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ambapo kwa mapenzi yake na wananchi wa Mkoa wa Tanga baada ya kuingia madarakani aliongeza bajeti ya barabara za TARURA kutoka Sh Bilioni 12.4 hadi Sh Bilioni 36.6 ndani ya mkoa huu.
Kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Handeni tunatekeleza mradi huu wa RISE ambapo km 105.1 zitajengwa kwa kiwango lami. Kwa sasa wahandisi washauri wapo kazini wanaendelea na kazi ya usanifu km 50 za awali,” Amesema Mhe Ndejembi.
Amesema barabara zitakazojengwa ni Mzundu-Kabiku km 17.6, Kwachaga-Kwamkonje km 10.1, Michungwani-Kwadoya km 18.8, Sindeni-Kwedikwazu km 37.7 na Mkata-Kwasunga km 21km.
Post A Comment: