Serikali ipo katika hatua za mwisho za kuwezesha upatikanaji wa Leseni Kubwa ya uchimbaji madini (Special Mining License – SML) kwa Kampuni ya Nyati Mineral Sand,inayomilikiwa na kwa ubia kati ya Serikali ya Tanzania na Kampuni ya Strandline,ambayo itapelekea kuanza kwa mradi mkubwa wa uchimbaji madini Tembo katika Wilaya ya Pangani Mkoani Tanga.
Hayo na Waziri wa Madini Anthony Mavunde alipofanya ziara ya kutembelea sehemu ya eneo la mradi huo iliyopo katika kijiji cha Stahabu, Kata ya Mikinguni Wilayani Pangani-Tanga.
“Mh. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameelekeza Wizara ya Madini kuhakikisha tunawezesha uanzishwaji wa miradi hii mikubwa na ya kimkakati ambayo itapelekea si tu ustawi wa uchumi wa Nchi yetu, bali kuwa kichocheo cha maendeleo na ustawi wa Wilaya ya Pangani na wananchi wanaozunguka mradi huu.
Ni dhamira ya Serikali yetu kuona wawekezaji wakubwa wenye nia njema na Nchi yetu kama hawa wanapewa ushirikiano ili kuwezesha shughuli zao kwa manufaa ya Taifa letu.
Mradi huu unatarajiwa kuwa na thamani ya dola za kimarekani milioni 125 ambao unakadiriwa kuishi kwa miaka 20 hadi 25 utatekelezwa katika Vijiji 8 vilivyopo katika Kata za Mikinguni, Mwera, Tungamaa na Bweni-Wilaya ya Handeni,Mkoani Tanga.
Nimefurahishwa na utayari wa wananchi wanaoguswa na mradi kupisha kuanza kwa mradi, na kwa kuwa ni hatua muhimu sana kwani itarahisisha kuanza mradi kwa wakati na kuondoa changamoto ya migogoro kati ya wananchi na mwekezaji”Alisema Mavunde
Akizungumza kwa niaba ya Mwekezaji, Mkurugenzi wa Kampuni ya Nyati Mineral Sand Ltd ambaye anawakilisha Hisa za Serikali, Ndg.Heri Gombera alieleza kwamba mradi huo unatarajiwa kuanza mwaka 2026 na unatarajiwa kuzalisha tani milioni 8 kwa mwaka ya madini mbalimbali yakiwemo titanium, ilmenite, rutile, zircon na monazite ambayo pamoja na matumizi mengine hutumika pia kuzalisha malighafi za injini za ndege,nyuklia,vifaa vya hospitali na viwanda vya marumaru na rangi.
Aidha, Bwana Gombera alitanabaisha kwamba Kampuni ya Nyati Minerals Sand ipo tayari kwa ajili ya kuanza kutekeleza mradi huo na kuongeza kuwa pindi watakapopata Leseni yao, kwa kushirikiana na Wadau wote wataanza zoezi la tathmini na ulipaji wa fidia kwa wananchi ili kupisha kuanza kwa mradi huo.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Pangani, Mh. Zainab Abdallah alimshukuru Mh.Rais Samia kwa kuendelea kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji nchini ambayo yamepelekea mradi huo kuanzishwa Wilayani Pangani. Na kwamba mradi huu utakapoanza utaleta manufaa makubwa kwa wananchi wa Pangani kuongeza kipato chao na kujikimu kutokana na ujira watakaokuwa wanaupata kutoka kwenye Mradi sambamba na kuchochea uchumi wa wilaya hiyo.
Post A Comment: