Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) imepokea msaada wa mtambo wa upasuaji wa ubongo kwa njia ya Matundu (ETV Tower) kwaajili ya upasuaji kwa watoto wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi wenye thamani ya Tsh 500 Millioni kutoka Taasisi ya Cure International.
Mkurugenzi Mtendaji wa MOI Prof Abel Makubi amesema vifaa hivyo vitasaidia watoto wengi zaidi kupata huduma ya upasuaji ambapo watoto wawili wataweza kufanyiwa upasuaji kwa wakati mmoja.
Amesema tangu kuanzishwa kwa huduma hiyo MOI miaka 13 iliyopita idadi ya watoto wanaofikishwa hospitalini hapo kwa matibabu imekuwa ikiongezeka na kwamba jitihada zaidi zinahitajika kuhamashisha wananchi kuwapeleka hospitalini watoto hao.
“Hapa nchini, inakadiriwa kuwa watoto 7,500 huzaliwa na matatizo ya vichwa vikubwa na mgongo wazi kila mwaka, kati ya hapo 1,500 tu ndiyo wanaoletwa hospitali kwa matibabu…hapa MOI tangu kuanza kutolewa kwa huduma hizo watoto 7,500 wamefanyiwa upasuaji, haya ni mafanikio makubwa ingawa juhudi zinahitaji kuwafikia watoto wengi zaidi”
Aidha ameishukuru Taasisi ya CURE kwa msaada kwa mtambo huo wa upasuaji na kuahidi kuendeleza ushirikiano baina ya taasisi hizo ili kuendelea kuokoa maisha ya watoto wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi nchini.
Kwa upande wake Meneja Mipango wa CARE Neuro, Joshua Menya amesema msaada huo umelenga kuongeza juhudi za MOI za kutoa huduma kwa watoto wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi.
“Miaka 13 iliyopita tulitoa mashine kama hii, na leo tumekuja kutoa mashine nyingine, kikubwa tumefurahishwa na huduma za MOI kusaidia watoto hawa ambao jamii wanawaona kama laana…katika ushirikiano wetu huu pia tulijikita katika kuwajengea uwezo madaktari na sasa ni muendelezo wa vifaa tiba” amesema Menya
Blandina Chande ni mhudumu wa watoto wenye vichwa vikubwa MOI, ametoa wito kwa vijana kuacha tabia ya kutelekeza watoto walemavu na kuwachia mzigo wa kulea wanawake ambao hawana uwezo wa kifedha.
“Watoto hawa wanalelewa na mama, baba ametoroka …hasa hawa baba vijana ni tatizo sana, niwakumbushe kuwa watoto ni zawadi tuwalee pamoja” amesema Chande
Post A Comment: