IMG_20240220_142009_744
Mkutano Mkuu wa 79 wa mwaka wa Baraza la Michezo ya Majeshi Duniani (CISM) kwa mwaka 2024 kufanyika Tanzania.
Lengo la baraza hilo ni kutumia shughuli za michezo na utimamu wa mwili kama njia ya kueneza amani duniani, huku tunu za baraza zikiwa ni kuhamasisha mshikamano, urafiki, heshima, usawa, uadilifu na ushupavu.
Akizungumza leo Februari 20, 2024 na waandishi wa habari jijini Dodoma, Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Mkutano huo Meja Jenerali Francis Mindi amesema mkutano huo utafanyika kwa muda wa siku saba kuanzia tarehe 12 Mei, 2024 hadi tarehe 19 Mei, 2024 na mkutano huo unatarajiwa kuhudhuriwa na wajumbe kutoka nchi zote 140 za wanachama wa CISM.
“Katika kutekeleza dhamira Kuu ya Baraza hilo, nchi wanachama hushiriki katika mashindano ya Majeshi ya Dunia ya michezo mbalimbali, mafunzo ya michezo, ikiwemo Mkutano Mkuu ambao hufanyika kila mwaka kwa njia ya mzunguko kwa uwakilishi wa kila bara. Kama nilivyotangulia kusema Mkutano huo Mkuu kwa mwaka huu utafanyika hapa nchini. ,” amesema Meja Jenerali Mindi.
Amesema sababu zilizopelekea Tanzania kuteuliwa miongoni mwa nchi 47 za wanachama wa CISM kutoka bara la Afrika ni kufuatia kuonekana kuwa na sifa stahiki kwa mujibu wa kanuni za CISM ikiwemo amani, ulinzi na usalama .
“Mbali na kuhudhuria mkutano, wajumbe pia watapata fursa ya kutembelea vivutio vyetu vya utali hapa nchini. Aidha, kwa kuzingatia kuwa huu ni ugeni wa Kijeshi, kwa kutambua mchango wa Wanajeshi kote duniani katika kuleta ukombozi katika nchi zao,
ugeni huo utapata fursa ya kutembelea Mnara wa kumbukumbu ya Mashujaa Mnazi Mmoja kwa ajili ya kutoa heshima na kuweka mashada ya maua.”
Amesema kutokana na matarajio ya ujio wa wageni nchi itakuwa na fursa adhimu ya kulitangaza Jeshi na Taifa kwa ujumla katika maeneo ya Kijeshi, kisiasa, kiuchumi na kijamii ikiwemo kuitangaza na kuendeleza lugha ya Taifa ya Kiswahili, ambayo itakuwa miongoni mwa lugha tano zitakazotumika kwenye Mkutano ikiwemo Kingereza, Kihispania, Kifaransa, Kiarabu pamoja na Kiswahili.
Tanzania ilikuwa mwenyeji wa mkutano mkuu wa CISM mwaka 1991 uliofanyika Jijini Arusha na mkutano kama huo wa aina yake uliacha kumbukumbu nzuri hasa kwa wageni kutembelea mbuga za wanyama za Manyara na Ngorongoro ‘Crater’.
Amesema Mgeni rasmi siku ya ufunguzi Mei 13, 2024 anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na siku ya kufunga Mei 17, 2024 mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa.
Kwa upande wa Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Michezo JWTZ, Kanali Martin Msumari amesema kutakuwa na michezo ya kipaumbele kama vile riadha,  mchezo wa ngumi na michezo mingine.
Amesema kupitia mkutano mkuu wa CISM ni njia pekee ya kuendeleza diplomasia kupitia michezo kwani CISM huwa inatoa mialiko kwa nchi zote za wanachama na wasio wanachama ambao hukutanisha nchi hizo kwenye michezo au mikutano ya kikatiba ikihudhuriwa na wakurugenzi wa michezo kutoka nchi mbalimbali.
Share To:

Post A Comment: