Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Madini Msafiri Mbibo ameitangaza na kueleza uwepo wa dhana ya Vision 2030: Madini ni Maisha na Utajiri kwa Uongozi wa Mji wa Chanthaburi nchini Thailand na kuwaeleza dhana hiyo imebeba fursa nyingi za Kiuwekezaji katika Sekta ya Madini.
Kufuatia hali hiyo, amewaalika wafanyabiashara kutoka mji huo kuwekeza Tanzania kwenye nyanja mbalimbali katika Sekta ya Madini nchini kutokana na Tanzania kubarikiwa utajiri wa rasilimali madini ambapo bado Serikali inahitaji ushirikiano katika maeneo mengi ya kiuwekezaji ikihusisha shughuli za utafiti, uongezaji thamani, teknolojia za kuchimba, mitaji na ushirikiano wa kibiashara.
Aidha, Mbibo ametumia fursa hiyo kuueleza uongozi wa mji huo pamoja na wafanyabiashara walioshiriki kikao hicho kuhusu dhamira ya Serikali kurejesha minada ya Madini ya Vito na Maonesho ya Vito ya Arusha na kufafanua kwamba, kwenye minada itakuwa mahali pekee ambapo Serikali itatoa nafasi ya kuuza madini ghafi baada ya kufanya marekebisho ya Sheria ambayo inataka madini kuongezwa thamani kabla ya kusafirishwa nje ya nchi.
‘’ Ni kwenye minada pekee ambapo wafanyabiashara watapata fursa ya kununua na kusafirisha madini ghafi ya vito. Nitumie nafasi hii kuwahamasisha wafanyabiashara kutoka hapa Chanthaburi kuitumia nafasi hii muhimu. Mhe. Gavana nafahamu wapo wafanyabiashara wengi wanaoingiza madini ya vito hapa Chathaburi kutoka maeneo mbalimbali duniani lakini napenda ufahamu kwamba, yapo mengi ambayo asili yake ni Tanzania.’’
Aidha, Mbibo ameieleza adhira hiyo kuwa, Serikali imepanga kuifanya minada hiyo katika taswira ya Kimataifa na viwango vya juu ambapo itashirikiana na na Sekta binafsi huku ikitarajiwa kuwa shindani na ya wazi na kuongeza na kuwa, sababu ya kufika katika mji huo ni kutokana na kupiga hatua katika shughuli mbalimbali zinazohusisha uongezaji thamani madini ya vito, biashara ya vito kwa lengo la kujifunza, kuomba na kuimarisha ushirikiano, kutangaza fursa za kiuwekezaji na kubadilishana uzoefu.
Aidha, Mbibo ametumia hadhira hiyo kuuomba uongozi wa mji huo kutoa nafasi kwa wafanyabiashara wa watanzania kujifunza kutoka katika mji huo na wale wa Chathaburi kujifunza Tanzania pamoja na kuuomba kutafakari namna ya kushirikiana na Tanzania kuwajengea uwezo watanzania walioko katika maeneo yenye shughuli kubwa za uchimbaji madini ya vito ili kubadilishana uzoefu kwa lengo la kujenga ari ya kuhamasisha vijana kujiingiza katika shughuli za uongezaji thamani madini kwa maendeleo ya sekta ya madini duniani.
Kwa upande wake, Makamu Gavana wa Chanthaburi Bw. Thawatchai Namsamut amekaribisha ushirikiano na Tanzania katika shughuli za madini ikiwemo kubadilishana taarifa na uzoefu utakaosaidia maendeleo ya sekta ya madini kwa pande zote.
Ameilezea Sekta ya Madini ya mji huo na kuongeza kwamba, soko la madini ya vito la Chanthaburi ndiyo soko kubwa la madini nchini Thailand na kwamba shughuli za madini zinazofanyika katika mji huo zimekuwa zikivuta wafanyabiashara kutoka maeneo mbalimbali duniani ambao wanaifanya Chantaburi kuwa kitovu cha biashara ya vito kwa walaji wa mwisho.
Serikali ya Mji huo pamoja na wafanyabiashara wa Chanthaburi wameipokea taarifa za urejeshwaji wa madini ya vito kwa ari kubwa na kuitaka Serikali iharakishe kutokana na mahitaji ya madini ya vito katika mji na nchi hiyo. Kihistoria, Chanthaburi ilikuwa maarufu kwa shughuli za uchimbaji madini ya vito nchini humo lakini miaka ya sasa shughuli hizo hazifanyiki tena. Kwa sasa biashara kubwa inayofanyika ni ya shughuli za uongezaji thamani madini ya vito ya thamani kubwa na biashara ya vito ambapo kwa kiasi kikubwa madini ghafi zinazoingizwa zinatoka katika nchi mbalimbali duniani ikiwemo Tanzania.
Katika ziara hiyo ya kikazi katika mji wa Chanthaburi, pia, Naibu Katibu Mkuu na ujumbe wake wamepata fursa ya kutemebelea katika viwanda vidogo vya uongezaji thamani madini kwa lengo la kujifunza na kuona namna shughuli hizo zinavyofanyika.
Post A Comment: