Tanzania na Thailand Zimesaini Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano kupitia Taasisi za Jemolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (TGC) na Taasisi ya Jemolojia, Vito na Usonara ya Thailand (GIT) inayolenga katika maeneo ya teknolojia za kisasa, kuongeza ujuzi, tafiti na uzalishaji wa bidhaa zenye Viwango vya Kimataifa zinazotokana na Madini ya Vito ya Thamani kubwa.

Imeelezwa kuwa kwa muda mrefu Tanzania imekuwa ikichimba na kuuza madini ya vito vya thamani kubwa yakiwa ghafi lakini kutokana na mabadiliko ya Sheria ya Madini inataka madini kuongezwa thamani kabla ya kuuzwa nje. Hivyo, makubaliano hayo ni moja ya hatua za utekelezaji wa matakwa ya Sheria pamoja na kuwandaa watanzania kushiriki katika uchumi huo. Inakadiriwa Tanzania inazalisha takriban aina 20 za madini ya vito .

Akizungumza baada ya kusaini makubaliano hayo Februari 22, 2024, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Madini Msafiri Mbibo ambaye anaongoza ujumbe wa Tanzania nchini humo ametoa wito kwa watanzania kuchangamkia fursa zilizopo katika sekta ya uongezaji thamani madini ya vito na kuacha kuamini kuwa uchimbaji au biashara ya madini ipo katika madini ya dhahabu pekee.

‘’ Ili kuuza bidhaa za mapambo nje kwenye masoko makubwa ya kimataifa ni lazima yafikie ubora wa viwango vya juu wa kimataifa hivyo, ushirikiano huu ni hatua ya kuwaandaa watanzania kutumia mawe ya thamani kutengeneza bidhaa zinazoweza kuuzwa popote Duniani. Makubaliano haya yameongeza uaminifu na ari ya ushirikiano kati yetu kwa ridhaa ya Serikali zetu mbili,’’ amesisitiza Mbibo.

Awali, Mbibo ametumia fursa hiyo kuwakaribisha nchini Tanzania wafanyabiashara wenye nia ya kuwekeza katika uongezaji thamani madini ikiwepo ukataji , uchongaji na unga’rishaji madini, utambuzi wa vito na shughuli nyingine za uongezaji thamani madini. Pia, ametumia jukwaa hilo kuhimiza jumuiya ya wafanyabiashara wa Thailand kushirikiana na wafanya biashara wa Tanzania kutafuta fursa zilizopo nchini.

‘’ Kiasi kubwa cha madini yetu ya vito bado yanauzwa nje ya nchi yakiwa ghafi, hivyo kuna fursa kubwa ya kuanzisha viwanda vya kutengeneza madini na bidhaa za vito,’’ amesema Mbibo.

Ameongeza kwamba, wazo la kuingia makubaliano hayo lilianzishwa na aliyekuwa Waziri wa Madini Dkt. Doto Biteko ambaye sasa ni Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati wakati wa ziara yake aliyoifanya nchini humo kwa mara ya kwanza mwaka 2022 na alipohudhuria Maonesho ya Vito ya mwaka2023.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa GIT Sumed Prasongpongchai amesema makubaliano hayo ni hatua kubwa kwa Tanzania katika tasnia hiyo na kuongeza kwamba taasisi hiyo iko tayari kuisaidia Tanzania na kuimarisha ushirikiano katika eneo hilo si tu kwa Tanzania bali katika maendeleo ya madini hayo duniani.

Mkurugenzi Mkuu wa GIT ameongeza kwamba, Tanzania ina madini na wao wana soko na teknolojia, hivyo ushirikiano huo utaleta faida kubwa kwa tasnia ya vito na bidhaa za usonara.

Ameeleza kuwa, dunia hivi sasa inaingia katika uhitaji wa bidhaa safi na salama, yaani zinazozalishwa bila kuhatarisha mazingira, haki za binadamu na kuepuka kusababisha machafuko na vita.

 

Naye, Kaimu Mratibu wa TGC Mhandisi Ally Maganga akizungumza katika mahojiano maalum amesema makubaliano hayo yamefungua ukurasa mpya kwenye tasnia ya uongezaji thamani madini nchini kutokana na ushirikiano huo kwa kuzingatia kwamba nchi ya Thailand imepiga hatua kubwa katika sekta hiyo.

Ameongeza hiyo ni kiashiria kuwa Serikali imedhamiria kuona sekta hiyo inakua kutokana na jitihada inazoendelea kuzifanya katika eneo hilo ikiwemo upanuzi wa miundombinu katika kituo cha TGC ambapo tayari jumla ya shilingi bilioni 30 zimetengwa na Serikali ili kukiimarisha kituo hicho.

‘’Hatua hii inadhihirisha dhamira ya Serikali kuboresha sekta ya uongezaji thamani madini ili kukidhi viwango vya kimataifa na kuongeza Mchango kwenye Uchumi. Hatua hii itafungua ukurasa mpya katika kukuza ajira lakini kuibua fursa mbalimbali zilizopo,’’amesema Maganga.

Share To:

Post A Comment: