Makamu mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Ngorongoro ambaye pia ni Diwani wa kata ya Olbalbal iliyopo ndani ya hifadhi ya Ngorongoro Mhe. Emmanuel Tonge ni miongoni mwa wananchi 463 waliohama kutoka ndani ya hifadhi ya Ngorongoro kwenda Kijiji cha Msomera na maeneo mengine.
Hafla ya kuwaaga wananchi wanaohama kwa hiari imefanyika leo tarehe 19 machi, 2024 na kuongozwa na mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro Kanali Wilson Sakulo ambapo jumla ya kaya 77 zenye watu 463 na mifugo 1,408 wamehama ndani ya hifadhi hiyo baada ya kujiandikisha kuhama kwa hiari.
Diwani wa kata ya Olbalbal ambaye pia ni Makamu mwenyekiti wa Halmashauri ya Ngorongoro na katibu wa baraza la wafugaji Ngorongoro amesema ameamua kuhama baada ya kuona dhamira ya Serikali ya awamu ya 6 kuboresha huduma bora za kijamii nje ya hifadhi na kurahisisha mazingira ya uandikishaji kwa kuwafuata wananchi kwenye ofisi za vitongoji, vijiji na kata kuwapatia elimu ya kutosha kuhusu uwepo wa maisha bora ndani ya hifadhi.
“Ndani ya hifadhi hakuna kesho iliyobora kwa watoto wangu, Serikali ikaona itenge maeneo rasmi na kujenga huduma za kijamii kama shule, vituo vya afya, zahanati, maji safi, barabara, mawasiliano ya simu, posta, majosho, eneo la malisho na mashamba ya kutosha kwa kilimo, kwa fursa hii sina haja ya kuendelea kushi na Wanyama ndani ya hifadhi” ameongeza Mhe. Tonge.
Meneja mradi wa kuhamisha wananchi wanaohama kwa hiari Ngorongoro Afisa Uhifadhi Mkuu Flora Assey ameeleza kuwa hadi kufikia wiki hii jumla ya kaya 1,195 zenye watu 7,195 na mifugo 33,064 zimeshahama ndani ya Hifadhi.
Ameongeza kuwa kati ya kaya 77 zilizohama ndani ya hifadhi wiki hii, kaya 75 zimeenda Kijiji cha Msomera Wilaya ya Handeni na kaya mbili (02) zimehamia kijiji cha Makao Meatu Mkoani Simiyu.
Naibu Kamishna wa Hifadhi huduma za Shirika NCAA Salum Mjema amebainisha kuwa Serikali imeendelea kuboresha zoezi la utoaji elimu, uandikishaji na uthaminishaji kwa kuongeza timu ya uandikishaji ambapo ndani ya mwezi mmoja taratibu zote ikiwepo malipo zinakuwa zimekamilika na wananchi kuhamishwa bila kusiburi mda mrefu.
Mjema ameongeza kuwa ujenzi wa nyumba za makazi 2,500 katika Kijiji cha Msomera unaendelea kwa kasi ambapo nyumba 903 zimeshakamilika, nyumba 97 zipo katika hatua za umaliziaji, nyumba 1500 zipo kwenye hatua mbalimbali za ujenzi huku maandalizi ya ujenzi wa nyumba zingine 2500 yakiendelea katika vijiji vya Kitwai Wilani Simanjiro na Saunyi wilaya ya Kilindi.
Katika hatua nyingine mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro Kanali Wilson Sakulo ametoa wito kwa jamii kupuuza baadhi ya watu wanaopotosha kuwa baadhi ya wananchi wanaohamishwa ndani ya hifadhi sio wakazi wa Ngorongoro na kusisitiza kuwa serikali iko macho na makini katika utekelezaji wa zoezi kwa kuhakikisha wananchi wote wanaojiandikisha kuhama kwa hiari ni wakaazi wenyeji wanaoishi ndani ya eneo la hifadhi ya Ngorongoro lenye vijiji 25 na kata 11 na si vinginevyo.
Post A Comment: