Mafanikio ya sekta ya Afya katika kukabiliana na kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi, mama na mtoto kumepelekea baadhi ya mataifa mengine ya Afrika kuja kujifunza nchini.
Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. John Jingu leo tarehe 22 Februari, 2024 Jijini Dodoma wakati wa kikao na wajumbe kutoka Serikali ya Nigeria uliongoozwa na Kamishina wa Afya wa jimbo la Borno Prof. Baba Gana, waliokuja kwa lengo la kujifunza njia za kupunguza vifo vya uzazi na mtoto kupitia mfumo wa M-mama.
Dkt. Jingu amesema mafanikio haya ambayo Serikali imeyapata ni kutokana na jitihada na bunifu mbalimbali katika kukabiliana na vifo vya mama na mtoto, na matokeo yameonekana na kufanya Tanzania kuwa sehemu iliyovutia mataifa mengine kuja kujifunza.
“Takwimu zinaonyesha mwaka 2015 vifo vya watoto wachanga vilikuwa ni 556 kati ya vizazi hai laki 100,000 namba hizi zimeshuka kufikia vifo 104 kwa vizazi hali laki 100,000 kwa hiyo wenzetu wakajiuliza tumefanyaje, tumewaambia hii ni kutokana na uongozi imara wa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassani ambae amekuwa ni kinara katika kuhakikisha afya za mama na mtoto zinalindwa kwa kuwa na miundombinu wezeshi na kufanya kazi kwa ubora kote nchini na kuwa na watumishi wanaofanya kazi kwa weledi. Amesema Dkt. Jingu.
Amesema Serikali imeweka mkakati wa kuzuia vifo vinavyotokana na uzazi mama na mtoto mchanga na kwamba havikubaliki kwa sababu njia za kuvizuia zipo na zinatekelezeka kwa kuwa na jitihada na ubunifu wa uzazi salama ambao unashirikisha jamii.
“Tanzania tuna mfumo mpya wa uzazi salama ambao kwa sasa uko katika Halmashauri 30 kwenye hatua za majaribio na baadae tutaendelea na awamu ya pili katika Halmashauri 110, lengo likiwa ni kuhakikisha wadau muhimu ambao ni jamii wanashirikishwa kikamilifu”. Amesema Dkt. Jingu.
Kwa upande wake Kamishna wa Afya jimbo la Borno Prof. Baba Gana amesema nchi ya Nigeria bado haijapiga hatua kwenye kuzuia vifo vinavyotokana na uzazi hivyo wamevutiwa na jitihada za serikali ya Tanzania na kuja kujifunza.
“Hakuna sehemu nzuri ya kwenda kujifunza kama kwa ndugu yako hivyo kutokana na hatua kubwa mliopiga kama taifa la Tanzania kwenye kupunguza vifo vya mama na mtoto ndio maana tumekuja kujifunza na kubadilishana uzoefu. Ni ukweli usio pingika kuwa sisi Nigeria bado hatujapiga hatua kweli hili, pia ujio wetu huu unakwenda kufungua milango ya mashirikiano ya mataifa haya mawili kwa ukaribu zaidi”. Amesema Prof. Baba
Post A Comment: