Na Mwandishi Wetu, KAMPALA
“Vitu lazima vitokee”, ni msemo ambao ameutumia Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba ,alipokutana na Mawaziri wenzake jijini Kampala, Uganda pembezoni mwa Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Nchi Zisizofungamana na Upande Wowote (NAM) na Mkutano wa Kundi la Nchi 77+China tarehe 15 hadi 22 Januari 2024.
Waziri Makamba ambaye alishiriki kwa siku tatu katika Mikutano hiyo alikutana na Mawaziri 17 kutoka nchi mbalimbali duniani kwa lengo la kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia na nchi hizo na kuweka mikakati ya kushirikiana kiuchumi kwa manufaa ya pande zote.
Waziri Makamba aliifanya Mikutano hiyo ambayo imekusanya takriban theluthi mbili ya nchi zote duniani kama fursa muhimu ya kuitangaza Tanzania kidiplomasia na kujadili mikakati na nyenzo za kujiletea maendeleo na kutatua changamoto zinazoikabili dunia.
Mawaziri wa Mambo ya Nje waliokutana na Mhe. Makamba wanatoka nchi za Kenya, Msumbiji, Somalia, Malawi, Misri, Ghana, Morocco, Filipino, Ethiopia, Singapore, Vietnam, Cuba, Iraq, Bahamas, Venezuela, Jamhuri ya Kidemokrsia ya Congo na Azerbaijan.
Masuala muhimu ambayo Waziri Makamba ameyasisitiza kwa mawaziri wenzake ni kutumia nyezo za kawaida za kidiplomasia kukuza ushirikiano baina ya mataifa yao. Nyenzo hizo ni pamoja na Midahalo ya Kisiasa, Tume za Pamoja za Kudumu za Ushirikiano (JPCs), Mikutano ya Majukwaa ya Kiuchumi, Tume za Pamoja za Mawaziri (JMCs) na ziara za viongozi wa kitaifa.
Mhe. Makamba amesema kuwa endapo vyombo hivyo vitatumika ipasavyo vitatoa fursa kwa pande husika kukuza biashara, uwekezaji, utalii pamoja na kutatua changamoto zinazoweza kujitokeza katika utekelezaji wa masuala ambayo pande husika zimekubaliana.
Wakati wa mazungumzo na Mawaziri wa nchi za Singapore, Vietnam na Filipino, Mhe. Makamba alisema nchi hizo ni mfano wa kuigwa na nchi zinazoendelea duniani kutokana na kupiga hatua kubwa ya maendeleo kwa kipindi kifupi.
Alikubaliana na mawaziri wa nchi hizo kushirikiana katika mafunzo, hususan, kueendeleza rasilimali watu, utalii na kilimo.
Jambo lingine lililojitokeza ni ushirikiano katika ujenzi wa miundombinu na usafiri wa anga wa moja kwa moja baina ya mataifa. Waheshimiwa Mawaziri walijiridhisha bila shaka kuwa ukosefu wa miundombinu unakwamisha ufanyaji wa biashara na kuongeza gharama katika uzalishaji, hivyo wamesisitiza kutumia rasilimali za nchi zao kujiletea maendeleo.
Aidha, Mhe. Waziri alisisitiza umuhimu wa kutafuta suluhu kwa njia za kidiplomasia panapotokea migogoro ya kisiasa na aliwahakikishia viongozi wenzake kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana na nchi nyingine katika utatuzi wa migogoro na ujenzi wa amani duniani.
Waziri Makamba katika kusimamia msemo wake wa “Vitu lazima vitokee” alikubaliana na viongozi wenzake kufufua makubaliano ya ushirikiano waliyojiwekea ili kuongeza kasi ya utekelezaji na kunzisha ushirikiano rasmi na nchi ambazo Tanzania haina mikataba rasmi ya ushirikiano
Post A Comment: