Ukosefu wa maji kwa wananchi na shule mpya ya Sekondari Masusu Wilayani Ngorongoro umepelekea wasimamizi wa mradi huo wa bweni kutumia zaidi ya milioni 22 kwaajili ya kununua maji ili kuendelea na ujenzi huo.
Aidha wananchi hao wametoa ombi kwa Wakala wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kuchimba kisima sambamba na uvutaji wa maji ya bomba ili kuondoa changomoto hiyo na wahusika kumalizia ujenzi wa shule ili wanafunzi waanze masomo
Ombi hilo lilitolewa kwa nyakati tofauti na wananchi hao akiwemo Yohana Kurito na Naskai Mollel wakati wa ziara ya Kamati ya Siasa mkoa wa Arusha, iliyotembelea na kukagua mradi wa ujenzi wa shule mpya ya Sekondari Masusu iliyopo kata ya Pinyinyi wilaya ya Ngorongoro, ikiwa ni ufuatiliaji wa utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2020 -2025.
Kurito alisema kukosekana kwa maji hayo kumepelekea wananchi hao kupitia Mkuu wa Shule ya Sekondari Sale,Ngunai Gidore ambaye ni msimaizi wa mradi wa shule hiyo kutumia sh,milioni 22 kununua maji wakati wa ujenzi
“Tunaiomba Ruwasa ivute maji hapa ili kupunguza gharama za tunazoingia serikali ilitoka sh ,milioni582.8 kwaajili ya ujenzi wa shule hii lakini katika hela hizo tumetumia sh,milioni 22 kununua maji kwaajili ya ujenzi wa shule hivyo Ruwasa watupe maji ya bomba na kuchimba kisima ili kuondoa changamoto hii “alisema Kurito
Naye Mwenyekiti wa CCM Mkoa,Loy Thomas ole Sabaya aliagiza Ruwasa chini ya Mhandisi wa wilaya hiyo, Gerald Andrew kuhakikisha ndani ya wiki moja shule hiyo inapata maji sambamba na uchimbaji kisima ili wananchi wa Pinyinyi na Masusu waweze kupata maji.
Pia wajumbe hao wa Kamati ya Siasa waliridhishwa na kuwapongeza viongozi na wananchi wa Masusu kwa usimamizi imara uliwezesha mradi huo kutekelezwa kwa viwango, licha ya kuwa umechelewa kukamilika kutokana na eneo hilo kukabiliwa na uhaba wa maji.
Huku Naskai Mollel alishukuru Rais Samia Hassan Suluhu kwa kuwajengea shule katika kata yao kwani uwepo wa shule hiyo itawasaidia watoto wao kupunguza mwendo wa kutembea zaidi ya kilomita 18 kwenda shule ya sekondari Sale.
Akiwasilisha taarifa ya mradi huo mkuu wa shule ya Sekondari Sale, Ngunai Gidore alisema mradi huo wa shule mpya ya sekondari Masusu umetekelezwa kwa gharama ya sh, milioni 584.2 fedha kutoka Serikali Kuu kupitia program ya SEQUIP.
Kiasi hicho cha fedha kilihusisha ujenzi wa vyumba 8 vya madarasa na ofisi mbili, jengo la utawala, maabara za fizikia, baiolojia na kemia, jengo la tehama, kichomea taka, tanki la kuhifadhia maji pamoja na vyoo vya wasichana, wavulana na wenye mahitaji maalum.
Post A Comment: