Jimbo la Kavuu lililopo halmashauri ya Mpimbwe wilaya ya Mlele mkoa wa Katavi katika kipindi cha kuanzia Novemba 2020 mpaka Februari 2024 limefanikiwa kutekeleza miradi ya elimu yenye thamani ya zaidi ya Tsh 9,986,388,189.47.
Hayo yamebainishwa na Mbunge wa Jimbo hilo na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe, Geophrey Pinda katika Mkutano Mkuu wa Jimbo la Kavuu wa kuwasilisha Taarifa ya Utekelezaji Ilani ya Chama cha Mapinduzi kuanzia Novemba 2020 hadi Februari 2024. Mgeni rasmi kwenye mkutano huo alikuwa Waziri Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe, Kassim Majaliwa Majaliwa.
Amesema, kati ya kiasi hicho cha fedha Tsh 6,849,553,942.86 zimetumika kujenga miundombinu ya madarasa, kukamilisha maboma, maabara na ujenzi wa shule mpya za msingi na sekondari huku Tsh 1,258,714,246.61 zikutumika kugharamia elimu bila malipo, mitihani na kulipa posho kwa walimu wanaojitolea wa masomo ya sayansi.
Aidha, Mhe, Pinda alisema katika kipindi hicho cha utekelezaji ilani ya CCM jimbo lake la Kavuu limeweza kuimarisha utoaji wa elimu Jumuishi kwa wanafunzi ambapo ndani ya jimbo hilo kuna shule 27 jumuishi zenye wanafunzi wenye mahitaji maalumu na kitengo kimoja kilichopo shule ya msingi Majimoto.
‘’ Jumla ya Wanafunzi wenye mahitaji maalum ni 219 yaani wavulana ni 133 Wasichana 86 na walimu 10 wakiwemo wanaume 6 na wanawake 4 na miundombinu inaendelea kuboreshwa kuhakikisha makundi yote ya watoto wanapata haki ya kupata elimu na katika mazingira wezeshi’’ alisema Mhe, Pinda.
Akizungunza katika mkutano huo, Waziri Mkuu Kasima Majaliwa Majaliwa ameeleza kuwa hatua iliyofikia kwenye sekta ya elimu ndani ya jimbo hilo kni nzuri huku akisisitiza kuwa lengo la mbunge wa jimbo hilo ni kuhakikisha wanafunzi wanaotembea umbali mrefu wanaepukana na adha hiyo.
“Wakati nilipotembelea jimbo hili siku za nyuma na kuzindua madarasa mapya nane ipo tofauti kubwa ya wakati huo na kipindi hiki ambapo sasa kuna shule nyingi na kubwa kama hii ya Mizengo Pinda Sekondari” alisema Mhe, Majaliwa.
‘’Mabadiliko ninayoyaona katika jimbo la Kavuu hususan kwenye sekta ya elimu sioni kama wana mpimbwe na kavuu kwa ujumla hamyaoni’’. alisema.
Amemuelezea mbunge wa jimbo la Kavuu kuwa, ni mahiri katika kuratibu mambo na kuwataka wanachama wa Chama Cha Mapinduzi katika jimbo hilo kumpa nguvu ili aweze kufanya kazi.
Aidha, Mbunge wa jimbo la Kavuu Mhe, Geophrey Pinda aligusia pia maboresho katika sekta ya afya na kueleza kuwa, wamefanikiwa kujenga na kuimarisha vituo vya kutolea huduma za afya (Kalista) ambapo ilani ya chama chake inatoa kipaumbele kujenga na kuimarisha vituo vya kutolea huduma za afya sambamba na ukamilishaji wa maboma ili kuweza kutoa huduma bora zaidi kwa wananchi ifikapo mwaka 2025.
Kwa mujibu wa Mhe, Pinda, kwa kipindi cha 2021 hadi 2024, Halmashauri ya Mpimbwe imeendelea na upanuzi wa hospitali ya Halmashauri kwa ujenzi wa wodi tatu za wagonjwa, Wodi ya upasuaji, wodi ya daraja la kwanza, jengo la upasuaji sambamba na ujenzi wa jengo la huduma za dharura katika hospitali ya wilaya.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe, Kassim Majaliwa Majaliwa akimueleza jambo Mbunge wa Jimbo la Kavuu Mhe, Geophrey Pinda alipokwenda jimboni kwake kwa ajili ya Mkutano Mkuu wa Jimbo la Kavuu tarehe 25 Februari 2024.Sehemu ya wajumbe na wageni waalikwa wakifuatilia uwasilishwaji Taarifa ya Utekelezaji wa Ilani ya CCM kutoka kwa Mbunge wa Jimbo la Kavuu halmashauri ya Mpimbwe mkoa wa Katavi Mhe, Geophrey Pinda tarehe 25 Februari 2024.
Mbunge wa Jimbo la Kavuu na Naibu Waziri wa Ardhi Mhe, Geophrey Pinda akiwasilisha Taarifa ya Utekelezaji Ilani ya Chama cha Mapinduzi kuanzia Novemba 2020 hadi Februari 2024 katika Mkutano Mkuu wa jimbo la Kavuu uliofanyika Shule ya Sekondari Mizengo Pinda katika halmashauri ya Mpimbwe mkoa wa Katavi tarehe 25 Februari 2024.
Post A Comment: