Kamishna wa Uhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania – TFS Prof. Dos Santos Silayo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Mkutano ya Kongresi ya 50 ya shirikisho la vyama vya wafuga Nyuki Duniani (APIMONDIA) ameongoza kikao cha kwanza cha kamati hiyo kilichofanyika katika ukumbi wa Misitu House, Itega jijini Dodoma.
Akizungumza leo Jumatano Februari 7, 2024 jijini Dodoma, mara baada ya kufungua kikao hicho, Prof. Silayo amesema kikao hicho ni sehemu ya maandalizi ya mkutano huo wa kihistoria utakaofanyika mwaka 2027 na kutarajiwa kuwakutanisha wadau wa Nyuki zaidi ya 6,000 jijini Arusha.
“Mkutano huu utawaleta pamoja wafugaji Nyuki, wafanyabiashara, wasafirishaji, wazalishaji wa mazao ya Nyuki, watumiaji wa bidhaa na huduma kama vile utalii wa Nyuki, uchavushaji mazao, huduma za matibabu ya Nyuki, watafiti na wanasayansi, wanafunzi, viongozi wa Serikali na watoa huduma mbalimbali” alisema Prof. Silayo.
Aidha Prof. Silayo amesema Sekta ya Nyuki Tanzania ipo tayari kwa mkutano huu na wadau kutoka sehemu mbalimbali ikiwemo sekta binafsi ni sehemu ya kamati ya maandalizi.
“Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki aliteua na kutoa maelekezo kwa kamati ya maandalizi kuhakikisha wadau wote wanashirikishwa ili kufanikisha Kongresi hii” Prof. Silayo.
Daniel Pancras, Kaimu Mkurugezi Msaidizi wa Maendeleo ya Ufugaji Nyuki, Wizara ya Maliasili na utalii, ambaye pia ni Katibu wa Kamati ya Maandalizi amesema kamati inajipanga vizuri na baada tu ya kikao hiki kazi itaanza kwa kasi kuhakikisha kongresi ya 50 ya APIMONDIA inakuwa ya kihistoria.
Mdau kutoka Sekta binafsi, Dkt. Judith Spendi, Mwenyekiti Mtendaji wa PMM, ameshukuru Serikali kwa kushirikisha sekta binafsi.
“Sekta binafsi tupo tayari, tutashirikiana bega kwa bega na Serikali kuhakikisha Kongresi ya 50 ya APIMONDIA inakuwa ya mafanikio makubwa” Dkt. Spendi.
Post A Comment: