KAMISHNA wa Ardhi Mkoa Arusha, Geofrey Msomsojo amezuia zoezi la utoaji hati za umiliki wa ardhi, katika eneo la ekari sita, lililopo kata ya Olmoti katika jiji hilo kutokana na eneo hilo kuwa na mgogoro kwa miaka 17 sasa, ikiwa ni utekelezaji agizo la siku 30 la Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Jerry Slaa.
Waziri Slaa wiki iliyopita, alitembelea eneo hilo na kuzungumza na William Mollel ambaye analalamika eneo lake kuvamiwa pamoja na majirani wa eneo.
Katika mgogoro huo, familia ya Mollel inamtuhumu aliyekuwa Ofisa Ardhi jiji la Arusha, Chritopher Kitundu ambaye hivi sasa amehamishiwa wilaya ya Tandahimba kuuziwa eneo na Leah Neeva hilo kinyume cha sheria.
Akizungumza na mwandishi wa habari hii, Kitundu alikana kuvamia eneo hilo na kueleza wanaomlalamikia waende mahakamani badala ya kumtuhumu kuvamia eneo lao.
“Mimi sijavamia eneo la mtu, kama kuna wanaonilalamikia basi waende mahakamani, ndipo haki inaweza kupatikana,” amesema.
Akizungumza katika kikao cha kutafuta suhulu ya mgogoro huo, Kamishna Msomsojo akiwa na Ofisa Ardhi wa mkoa huo, Neema Uloma amesema ameamua kusitisha utoaji hati wa viwanja katika eneo hilo, hadi suluhu itakapopatikana.
Amesema katika kutekeleza maagizo ya Waziri, Slaa juzi (Jumatatu) akiwa na maafisa wake, watafika tena katika shamba lenye mgogoro na kuzungumza na pande zote wakiwemo majirani ambao nao wanalalamika kumegwa ardhi yao.
“Tumepata taarifa kupimwa kwa eneo hilo na maafisa wetu wa ardhi licha ya kuwepo mgogoro na kuanza kuuzwa viwanja taratibu za kinidhamu zinaendelea na sasa tumesitisha utoaji wa hati,” amesema.
Awali Mollel amesema kwa miaka 17 wamekuwa katika mgogoro huo, baada ya Neeva Savoroi kuvamia shamba hilo ambaye tayari alifariki na baadaye mkewe Leah Neeva kuendelea kulimiliki kinyume cha sheria na kumuuzia Kitundu.
Amesema suala hilo limefikishwa Baraza la Ardhi la Kata kwa shauri namba S/2006 ambalo alishinda na baadaye shauri kuhamishiwa baraza la ardhi wilaya na baada ya kukata rufaa mahakama ya rufaa, shauri hilo lilirejeshwa baraza la ardhi.
“Hata hivyo wakati shauri lipo bado katika baraza la ardhi, Kitundu alitumia maafisa wenzake wa ardhi, kwenda kupima eneo hilo na kukata viwanja ploti namba 60-70 Block A, Plan No E/248/205 mnano Agosti mwaka jana,” amesema.
Amesema baada ya tukio hilo, walipeleka malalamiko baraza la ardhi na ofisi za Serikali kata ya Olmoti, ambao walifika shambani na kuagiza kusitishwa upimaji lakini maafisa hao walikaidi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa baraza la ardhi kata ya Olmoti, Yusuph Abdalah amekiri kuwepo na shauri la mgogoro huo, hata hivyo, amesema mlalamikiwa aliyeuza eneo hilo, Leah Neeva ameandika barua kutokuwa na imani na baraza na hivyo hatashiriki katika shauri hilo.
“Hili shauri bado lipo hapa, kwetu lakini Mlalamikiwa amekuwa hafiki kwenye vikao vya baraza na tayari ameandika barua rasmi kutokuwa na imani na baraza la ardhi,” amesema.
Hata hivyo, Neeva akizungumzia eneo hilo, ameeleza ni eneo la familia yake na waliuziwa na Mollel (ambaye analalamika kuvamiwa) miaka ya nyuma.
Post A Comment: