Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) wakiongozwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Deus Sangu leo Tarehe 12 Machi, 2024 wametembelea Mradi wa Kusambaza Umeme Vijijini wa REA III (Awamu ya Pili) katika kijiji cha Masware, Halmashauri ya wilaya ya Babati mkoa wa Manyara na baadae kijiji cha Miswakini Juu katika Halmashauri ya wilaya ya Monduli na kuupongeza Uongozi wa Wakala (REA) kwa ufanisi katika uratibu na usimamizi wa usambazaji wa nishati ya umeme kwa Wananchi wa vijijini.


Akiongea kwa niaba ya Wajumbe wa Kamati ya PIC; Mhe. Sangu ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo wa Kwela mkoani Rukwa amesema, Viongozi wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) wamesimamia vyema jukumu la kuhakikisha nishati ya umeme inafika katika vijiji vyote na kuongeza kuwa hapo awali, jukumu hilo lilionekana kuwa gumu na lisingetekelezwa kwa wakati ambapo hadi Mwezi Machi, 2024 vijijini 11,837 vimefikiwa na nishati ya umeme ukilinganisha na vijiji 12,318 vya Tanzania Bara, idadi hiyo ni sawa na asilimia 96 ya lengo.


Mhe. Sangu amesema Kamati ya PIC imejionea namna ambavyo Wananchi wameonyesha kuipokea Miradi ya nishati vijijini na kwamba mapokeo ni mazuri na kwamba fedha nyingi zilizowekwezwa na Serikali kwenye Miradi ya REA vijijini zimefika.


“Nimefarijika kuona Miradi ya REA ilivyopokelewa vizuri na Wananchi, wameongea wenyewe namna wanavyofaidika; mfano tumeona umeme ulivyosaidia kwenye kituo cha afya cha Masware na kwenye mashine ya kusindika nafaka, malalamiko ya Wananchi ni machache sana zaidi ya yote Wananchi wanahitaji kuongezwa kwa wigo wa utoaji wa huduma ya umeme”. Amekaririwa Mhe. Sangu, Mwenyekiti Kamati ya PIC.


Awali Wajumbe wa Kamati ya PIC walitembelea kijiji cha Masware katika kituo cha afya cha Masware pamoja na kujionea namna Wanakijiji wanavyonufaika na umeme kwenye eneo la huduma za afya pamoja na usindikaji wa mazao kwenye kiwanda kidogo cha kusindika nafaka katika kijiji hicho.


Baadae Wajumbe wa Kamati hiyo walitembelea kijiji cha Miswakini Juu na kwenye shule ya sekondari ya Miswakini, Halmashauri ya wilaya ya Monduli ambapo huduma ya umeme imefika kwenye shule hiyo.

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Hassan Saidy, aliwaeleza Wajumbe wa Kamati hiyo kuwa mkoa wa Manyara una jumla ya vijiji 441 ambapo kati ya hivyo, vijiji 420 vimeshafikiwa na huduma ya umeme, huku  vijiji 14 vipo kwenye hatua za mwisho za majaribio kabla ya kuwashwa muda wowote kuanzia sasa na kuongeza kuwa ni vijiji 7 tu, ndiyo vimebaki ambavyo vinataji kuwashwa kabla ya mwezi Juni, mwaka huu wa 2024.


Mhandisi, Saidy amesema, mkoa wa Arusha una jumla ya vijiji 368, vijiji 352 sawa na asilimia 95 vimefikiwa na huduma ya umeme huku vijiji 16 tu vikitarajiwa kukamilika kabla ya mwezi Juni, 2024 ambapo ameahidi Wakala (REA) itaendelea kuwasimamia Wakandarasi wote, wanaotekeleza Mradi wa REA (Mzunguko wa II) katika mkoa wa Arusha, ili wakamilishe jukumu hilo kwa wakati.

 

Katika ziara hiyo, msafara wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) uliongozwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB); Mhe. Balozi na Meja Jenerali Mstaafu, Jacob Kingu, Mkurugenzi Mkuu, Mhandisi, Hassan Saidy, Mkurugenzi wa Umeme Vijijini, Mhandisi, Jones Olotu pamoja na Menejimenti ya Wakala, hata hivyo ratiba ya ziara hiyo inatarajiwa kukamilika kwesho ambapo Kamati hiyo ya PIC, itahitimisha ziara hiyo, mkoani Arusha.




























Share To:

Post A Comment: