Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Joseph Mhagama ameipongeza Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa kubuni mifumo mbalimbali ya TEHAMA kwa lengo la kuboresha utendaji kazi serikalini.

Dkt. Mhagama amesema hayo leo Machi 16, 2024 Jijini Dodoma wakati Kamati hiyo ilipotembelea Ofisi ya Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, Sekretarieti ya Ajira na Tume ya Utumishi wa Umma kwa lengo la kupokea taarifa ya miradi mbalimbali inayotekelezwa na taasisi hizo. 

Aidha, kwa niaba ya Kamati, Dkt. Mhagama ameipongeza Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kupitia taasisi zake kwa kufanya kazi kubwa ya kubuni na kusanifu mifumo ambayo ni muhimu na yenye lengo la kuongeza ufanisi wa utendaji kazi Serikalini.

“Tulizoea kuona nchi za wenzetu zikibuni na kusanifu mifumo mahususi ya TEHAMA kwa maendeleo ya mataifa yao na wakati mwingine kutuuzia na sisi lakini leo tumesikia na kuona kwa macho yetu uwezo mkubwa wa vijana wetu wa ndani ya Serikali ambao wameunda mifumo muhimu kwa ajili ya Serikali yetu, hakika haya ni mapinduzi makubwa yatakayoleta ufanisi unaozingatia haki na wajibu Serikalini” alisema Dkt. Mhagama.

Kadhalika Dkt. Mhagama ameisisitiza Ofisi ya Rais-UTUMISHI kuhakikisha mifumo yote ya TEHAMA iliyopo na inayoendelea kubuniwa na kusanifiwa inakuwa endelevu ili kuboresha utoaji wa huduma kwa umma kwa njia ya TEHAMA.

Kwa upande wake Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete ameishukuru Kamati hiyo kwa kupanga ziara hiyo muhimu na kutoa maelekezo ambayo yatafanyiwa kazi kwa haraka na kutoa mrejesho.

Mhe. Kikwete ameongeza kuwa mifumo yote ikiwemo HCMIS, PEPMIS HR Assessment na mifumo mingine inatumika kwa ufanisi ili kutatua changamoto mbalimbali za kiutumishi kwa wakati.







Share To:

Post A Comment: