Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imekagua utekelezaji wa miradi ya usambazaji umeme vijijini inayotekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini ( REA) mkoani Pwani.
Mara baada ya ukaguzi huo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Dkt. David Mathayo ameishauri Serikali kuangalia gharama za uunganishaji umeme kwa wananchi wanaoishi katika maeneo yanayotambulika kama Vijiji Miji ili kuwawezesha wananchi wengi zaidi kuunganisha umeme kwenye maeneo yao.
Ameshauri kuwe na usawa wa gharama za uunganishaji umeme kati ya wananchi wa vijijini na Vijiji Miji kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo za kiuchumi.
Dkt. Mathayo ameyasema hayo tarehe 18 Machi, 2024 mkoani Pwani ambapo katika ukaguzi huo, Kamati iliambatana na Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Dkt. James Mataragio.
Naibu Waziri wa Nishati Mhe. Judith Kapinga amewashauri wakazi wa vijijini kutumia umeme kwa shughuli za maendeleo na kuchangamkia uunganishaji wa umeme kwenye maeneo yao mara baada ya Serikali kufikisha miundombinu ya umeme.
Kapinga amesema wakazi wa vijijini hulipia gharama za umeme wa REA kwa shilingi 27,000 baada ya Serikali kulipia gharama nyinginezo huku wakazi wa Vijiji Miji wakilipia shilingi 320,000 sawa na wakazi wa mijini.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dkt. James Mataragio alitoa rai kwa wananchi vijijini kuchangamkia fursa ya kuunganishiwa umeme kwa bei ya chini kwani Serikali inatumia fedha nyingi kuhakikisha umeme unafika kwenye maeneo hayo.
Awali Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Mhandisi Hassan Saidy alisema zaidi ya shilingi Bilioni 44 zimetumika katika kutekeleza miradi ya REA na kufanikisha kusambaza umeme katika vijiji zaidi ya 100 kati ya vijiji 110 vilivyopo mkoani Pwani.
Post A Comment: