MBUNGE wa Singida Mashariki Miraji Mtaturu amefanya ziara ya kutembelea eneo la ujenzi wa Kituo cha Polisi Kata ya Mkiwa na kutoa kiasi cha Shilingi Milioni 5 ili kuanzisha upya ujenzi huo ambao ulikwama kwa takribani miaka 13.

Lengo la kufanya hivyo ni kusogeza huduma za ulinzi na usalama karibu na wananchi kutokana na umbali mrefu uliopo mpaka kufika Makao Makuu ya Wilaya.

Kabla ya kutembelea eneo hilo akiwa ameongozana na Mkuu wa Polisi Wilaya ya Ikungi (OCD),Suzana Kidiku,Mbunge Mtaturu alifanya kikao na Uongozi wa Kata na Wadau wa Maendeleo wanaopatikana kwenye Kata hiyo.

Akizungumza katika kikao hicho Mtaturu ameuomba uongozi wa Kata kuwaalika wadau waliopo waweze kushirikiana kujenga Kituo hicho.

“Tuhamasishe wadau waje kutuunga mkono ili tufike kwenye renta tuweze kuishawishi serikali kukamilisha zaidi,niwashauri pia muunde kamati ya ujenzi ili kupanua wigo wa ushirikishaji wananchi na wadau,”.amesema.

Akizungumza kwenye kikao hicho OCD Suzana amemshukuru sana Mhe Mbunge kwa kuendelea kuwa mdau mkubwa wa usalama kutokana na ushiriki wake wa muda wote katika kusaidiana na Jeshi la Polisi ili kuimarisha utendaji kazi wao.

“Tuliposhirikishwa na Mbunge kuhusu ujenzi wa kituo hiki tuliandaa ramani na kuikabidhi katika uongozi wa Kata,niwahakikishie kutoa ushirikiano wetu unaostahili ili kukamilisha ujenzi wa kituo hiki cha Polisi cha Mkiwa,”amesisitiza.

Ametumia fursa hiyo kufikisha kwa mbunge,salamu za Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP),Camillius Wambura kwa juhudi zake za kusaidiana na Jeshi la Polisi kutimiza majukumu yao ikiwemo kuweka mazingira mazuri ya kufanyia kazi kwa askari wa Ikungi.

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Mkiwa ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Ikungi Petro Mtiana amemshukuru Mbunge kwa kuendelea kuwajali wana Mkiwa kutokana na miradi mbalimbali ya maendeleo inayoendelea kutekelezwa.

“Hapa tumeendelea kupokea fedha nyingi za maendeleo,hivi karibuni tumepokea fedha za kukamilisha ujenzi wa madarasa manne katika Sekondari ya Mkiwa,na tumekamilisha chumba kimoja cha maabara,na kama hiyo haitoshi tumepokea pia Shilingi Milioni 46 za kujenga vyumba viwili vya madarasa,

“Naomba tupelekee salaam zetu za pongezi na shukrani kwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kusikia kilio chetu na kutuletea fedha nyingi za maendeleo kwenye Kata yetu ya Mkiwa,nikuhakikishie Mbunge wetu na OCD kuwa tutawaunga mkono katika ujenzi wa kituo hiki kwani kukamilika kwake kutawahakikishia wananchi usalama wao na mali zao kwa kuwa Kata hiyo ipo mpakani mwa wilaya Manyoni na Ikungi,”.amesema Diwani Mtiana.

 

Share To:

Post A Comment: