Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi imechangia takribani milioni 72 katika ujenzi wa jengo la Zahanati ya Kijiji cha Kweisewa kilichopo Wilayani Korogwe Vijijini Mkoani Tanga.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) katika ufunguzi wa jengo hilo uliofanyika Kijiji cha Kweisewa Wilayani humo.
“Mradi huu ulitengewa kiasi cha Shilingi milioni 73.8 hata hivyo wakati wa utekelezaji jumla ya Shilingi milioni 72 zilitumika hivyo nipongeze viongozi wa Hifadhi ya Taifa Mkomazi na Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe kwa kusimamia vyema matumizi ya fedha za umma” Mhe. Kairuki amesisitiza.
Waziri Kairuki amefafanua kuwa ujenzi wa Zahanati hiyo unatokana na fedha zilizotokana na mapato ya Utalii hasa baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kutangaza utalii kupitia Programu ya Tanzania the Royal Tour ambapo mapato yameongezeka kutoka Dola za Marekani Bilioni 2.5 kwa Mwaka 2022 hadi kufikia Dola za Marekani Bilion 3.34.
Amesema mafanikio hayo yameiwezesha Hifadhi ya Taifa Mkomazi kwa mwaka wa fedha 2023/2024 kuweza kurejesha/kuchangia kiasi cha Shilingi 765,080,368.88 katika miradi ya jamii kama ni faida ya jamii inayozunguka hifadhi ikiwemo ukamilishaji wa Zahanati ya Kweisewa na Ujenzi wa Kituo cha Polisi Kalalani (Korogwe), ujenzi wa bweni la Wavulana Shule ya Sekondari Kigonigoni na ujenzi wa Madarasa Mawili Shule ya Msingi Mgirigiri (Mwanga), ujenzi wa bweni la Wasichana Shule ya Sekondari Kalemawe (Same) na uchimbaji Kisima cha maji Kijiji cha Kivingo (Lushoto).
Ametumia fursa hiyo kuwaasa wananchi kutunza jengo hilo pamoja na samani zake ili lengo la kujengwa Zahanati hiyo la kutoa huduma bora kwa wananchi litimie.
Naye, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii na Mbunge wa Korogwe Vijijini, Mhe. Timotheo Mnzava amemshukuru Rais Samia kwa kuwezesha upatikanaji wa fedha za utalii hatimaye kufanikisha ujenzi wa zahanati hiyo.
“Tunamshukuru Rais Samia kwa sababu Zahanati hii isingeweza kujengwa endapo TANAPA haikusanyi mapato, ametangaza utalii, idadi ya watalii imeongezeka na mapato ya TANAPA yameongezeka” Mhe. Mnzava amesisitiza.
Kwa upande wake Kamishna wa Uhifadhi Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Bw. Musa Nassoro Kuji amesema kuwa Mradi huo umetekelezwa na Hifadhi ya Taifa Mkomazi kwa kushirikiana na wananchi wa Kweisewa na Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe.
Aidha, amesema mradi huo umejengwa kusaidia upatikanaji wa huduma za afya kwa wakazi waliokuwa wakitembea kwa zaidi ya kilomita 30 kufuata huduma za matibabu na pia utatoa hamasa kwa wananchi kushiriki katika shughuli za uhifadhi.
Akizungumzia changamoto ya wanyama wakali na waharibifu, Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, Mhe. Wiliam Mwakilema amesema ni vyema wananchi wakaangalia maeneo wanayopanga kwa matumizi ya kibinadamu yasiingiliane na mapito ya wanyamapori wakali na waharibifu.
Uzinduzi huo umehudhuriwa na Viongozi kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe, Mkuu wa Hifadhi ya Mkomazi na Watumishi wa Mkomazi, Wakuu wa Idara, Viongozi wa Vyama vya Siasa, Waheshimiwa Madiwani wa Halmashauri ya Korogwe na Viongozi wa kidini.
Post A Comment: