MKUU wa Mkoa wa Arusha mheshimiwa John Mongella amewahakikishia wananchi wanaohama kwa hiari kutoka ndani ya hifadhi ya Ngorongoro kwenda maeneo mengine nje ya hifadhi kuwa serikali imejipanga na hakuna mwananchi yoyote atakayekosa haki zake iwapo ataamua kuhama kwa hiyari.
Mheshimiwa Mongella ametoa kauli hiyo wilayani Ngorongoro Mkoani Arusha leo tarehe 25 Januari, 2024 wakati akiwaaga wananchi 818 walioamua kuhama kwa hiyari kutoka ndani ya hifadhi hiyo na kwenda kuishi katika Kijiji cha Msomera wilayani Handeni Mkoani Tanga.
Ameeleza kwamba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt .Samia Suluhu Hassan ametoa fedha za kutosha ili kuhakikisha kuwa zoezi hilo linafanikiwa na hakuna mwananchi yoyote atakayekosa kulipwa haki zake zote zilizoanishiwa katika utekelezaji wa zoezi hilo.
Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa ameongeza kuwa zoezi hilo linatekelezwa kwa kuzingatia misingi yote ya haki za binadamu ikiwemo kuboresha maisha ya wananchi hao wanapofika katika Kijiji cha Msomera wilayani Handeni Mkoani Tanga.
Kwa upande wake Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro bwana Richard Kiiza amesema kumekuwa na muamko na ari kubwa ya wananchi kujiandikisha na kutaka kuhama kwa hiyari ambapo katika tukio hilo jumla ya kaya 118 zenye watu 818 na mifugo 3,129 wamehama kwenda Kijiji cha Msomera.
Mratibu wa zoezi hilo la kuhamisha watu kutoka Hifadhi ya Ngorongoro bwana Fedes Mdalla amesema uhamisishaji wa wananchi kuhama ndani ya hifadhi unaendelea na zoezi hilo litakuwa linafanyika kila mara kulingana na idadi ya nyumba zinazoendelea kujengwa na kukamilika katika eneo la mradi.
Baadhi ya wananchi walioamua kuhama kwa hiyari kwenda katika Kijiji hicho wameishukuru serikali kutokana na jinsi inavyozingatia utu na maslahi ya kila mmoja katika kuhakikisha kuwa wanapata stahiki zao.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi hao Bw Sindato Ngenyike na Bi Theresia Sabore Moko wamesema kitendo cha wao kuondoka ndani ya hifadhi kimetokana na elimu waliyoipata kutoka kwa serikali na wananchi wenzao ambao tayari wameshamia katika Kijiji cha Msomera.
Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro inaendelea kuelimisha, kuandikisha na kuhamisha wananchi kutoka ndani ya hifadhi hiyo kila wiki ikiwa ni zoezi lenye lengo la kuboresha maisha ya wananchi na pia kulinda na kuimarisha hifadhi.
Post A Comment: