Na. Jacob Kasiri – Serengeti.

Kamishna wa Uhifadhi – TANAPA Musa Nassoro Kuji amesema kuwa hakuna eneo korofi la barabara litakalosalia bila kukarabatiwa ndani ya Hifadhi ya Taifa Serengeti ili kutatua changamoto zilizojitokeza hivi karibuni za kuharibika kwa miundombinu hiyo kulikosababishwa na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha nchini na nchi jirani na kuleta adha kwa watalii.

Kamishna huyo anayesimamia Hifadhi za Taifa 21 nchini ameyasema hayo jana Februari 08, 2024 wakati akifuatilia maagizo yake aliyoyatoa Januari 26, 2024 kwa menejimenti ya Hifadhi ya Taifa Serengeti ya kukarabati maeneo korofi ili kuondoa adha itokanayo na kuharibika wa barabara kutokana na  mvua kubwa zinazoendelea kunyesha nchini.

“Tunatambua umuhimu wa barabara katika Hifadhi za Taifa ikiwemo hii ya Serengeti ambapo hivi sasa hali ya barabara zetu inaendelea kuimarika na tumehakikisha tunaweka nguvu kubwa ili kufikia maeneo yote korofi na kwa kasi tuliyonayo tumebakiza maeneo machache tu ambayo ukarabati wake haujakamilika ila unaendelea na tunaimani katika kipindi kifupi kijacho ukarabati huu utakamilika”.

Aidha, Kamishna Kuji alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano  wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha kwa ajili ya ununuzi wa mitambo mbalimbali ya ujenzi ambayo imesaidia kurahisisha shughuli za ujenzi na ukarabati wa miundombinu hiyo pindi inapoharibika.

Naye, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi anayeshughulikia miundombinu Mhandisi Dkt. Richard Matolo alieleza kuwa licha ya ukarabati huu tunaoufanya, bado TANAPA ina mpango endelevu wa kuziboresha barabara hizi kwa kuziinua juu ili kuruhusu mtiririko wa maji kutoziharibu barabara hizi hususani nyakati za mvua nyingi.

Mhandisi Dkt. Matolo alisema, “Tumeanza  kukarabati maeneo korofi kwa kufukia mashimo,  kuweka mitaro ya kutiririsha maji barabarani lakini bado tuna mpango wa muda mrefu wa kumaliza kabisa changamoto ya barabara zetu kwa kuziinua na kuziwekea tabaka gumu litakalodumu kwa muda mrefu bila kuharibiwa na mvua.”

Aidha, Kamishna Matolo aliongeza kuwa, “Tutaanza utekelezaji wa  ujenzi wa barabara ya Seronara – Naabi – mpaka Golini yenye urefu wa kilometa 68 hivi karibuni, ambapo ujenzi huo utahusisha kujaza kifusi kwa ajili ya kuinua barabara, ujenzi wa vivuko, uchimbaji wa mitaro ya kupitisha maji na kuweka tabaka gumu almaarufu “Gravel Wearing Course”.

TANAPA inaendelea na ujenzi pamoja na ukarabati wa miundombinu ya barabara zilizoharibiwa na mvua ziweze kupitika vizuri licha ya uwepo wa mvua kubwa zinazoendelea kunyesha.

 

 

 

 

 

 

 

Share To:

Post A Comment: