Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango ametoa wito kwa washiriki wa Mkutano wa 21 wa Taasisi za Fedha kutafakari kwa kina changamoto ya uhaba wa fedha za kigeni na hatua gani za muda mfupi na wa kati zinazopaswa kuchukuliwa zaidi ya hatua za urekebu zinazochukuliwa na Benki Kuu ya Tanzania.
Makamu wa Rais amesema hayo wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa 21 wa Taasisi za Fedha unaofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC). Amesema ni muhimu kwa Mkutano huo kujadili nafasi ya kutumia viwango nyumbufu vya ubadilishanaji fedha (exchange rate flexibility) katika kudhibiti uhaba huo wa fedha za kigeni.
Aidha Makamu wa Rais amewataka viongozi na wataalam katika sekta ya fedha nchini kuhakikisha uwezo wa taasisi zao na sekta nzima unaimarika zaidi ili kuhimili misukosuko inapotokea. Amewasihi kuangalia namna ya kuimarisha zaidi Idara na vitengo vya utafiti na masoko ya kifedha nchini. Amesema Menejimenti ya vihatarishi, usimamizi makini na ufuatiliaji wa mwenendo wa benki moja moja na sekta nzima ni jambo la muhimu sana katika kujenga sekta ya fedha iliyo imara na yenye uwezo wa kuhimili misukosuko.
Halikadhalika Makamu wa Rais amesema Mkutano huo unapaswa kuangazia njia za kudhibiti mikopo chechefu, kupunguza gharama za mikopo na kupanua wigo wa mikopo nafuu hasa kwa wajasiriamali wadogo na wa kati katika sekta za kilimo, mifugo, uvuvi, uchimbaji wa madini na viwanda vidogo. Pia amesema sekta ya fedha inao wajibu wa kushiriki katika jitihada za kuhifadhi mazingira na kudhibiti athari za mabadiliko ya tabianchi kwani huathiri uzalishaji na mapato hususan katika sekta ya kilimo, utalii, ufugaji na hata uzalishaji katika viwanda vinavyotegemea malighafi zinazotokana na kilimo, misitu na maliasili.
Makamu wa Rais ametoa wito kwa taasisi zote za fedha kuimarisha jitihada za kudhibiti madhara yanayoweza kujitokeza kutokana na ukuaji wa kasi wa teknolojia ikiwa ni pamoja na changamoto za utunzaji na usiri wa taarifa, usalama wa mtandao wa kibenki, usambazaji wa taarifa potofu mitandaoni, udhibiti wa fedha haramu pamoja na kuwalinda watumiaji kwa kushirikiana kwa karibu na wadau wote.
Vilevile Makamu wa Rais amesema sekta ya fedha nchini kwa kiwango cha kuridhisha imeweza kuhimili misukosuko ya kiuchumi iliyojitokeza katika miongo miwili iliyopita na kupata mafanikio mazuri. Amesema takwimu rasmi za maendeleo ya sekta ya fedha nchini na tathmini ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) ya Disemba 2023 vinathibisha hivyo. Ametaja kwamba sekta kibenki iko imara na ina mtaji na ukwasi wa kutosha huku inatengeneza faida. Ukuaji wa mikopo iliyotolewa na mabenki kwa sekta binafsi umeongezeka kutoka 9.9% mwaka 2021/22 hadi 22.2% mwaka 2022/23. Halikadhalika, uwiano wa mikopo kwa sekta binafsi na Pato la Taifa ulifikia wastani wa 18.2% katika mwaka 2021/22 ikilinganishwa na 17.6% mwaka 2020.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Fedha Mhe. Hamad Chande amesema Serikali kupitia Wizara ya Fedha imeendelea kutekeleza jukumu muhimu katika juhudi za kuimarisha sekta ya fedha kulingana na mpango mkuu wa maendeleo ya sekta ya fedha wa mwaka 2020/2021-2029/2030. Pia amesema Wizara ikiwa msimamizi mkuu wa sera za kiuchumi inashirikiana kwa karibu na wadau wa sekta ya fedha kuendeleza hatua zinazokusudia kuimarisha sekta ya fedha kwa kutunga na kutekeleza sera zinazoboresha mazingira ya udhibiti, kuimarisha mfumo wa viashiria hatarishi na kukuza uwezo wa ndani wa sekta ya fedha.
Aidha Chande ameongeza kwamba Sekta ya Fedha ya Tanzania imeonesha uvumilivu katika kupambana na changamoto za uchumi wa dunia za hivi karibuni. Amesema ufanisi huo unajionesha katika ukuaji wa rasilimali hasa mikopo kwa sekta binafsi ambayo iliweza kukua kutokana na teknolojia za kifedha za hali ya juu na hatua zilizochukuliwa na Serikali pamoja na Benki Kuu za kuimarisha uchumi wa Taifa.
Akizungumzia uzinduzi wa Mfumo wa Taifa wa Malipo ya Papo kwa Hapo (Tanzania Instant Payments System) Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania Emmanuel Tutuba amesema uzinduzi wa mfumo huo unathibitisha dhamira ya serikali ya awamu ya sita ya kutumia ipasavyo mifumo ya kielektroniki katika kurahisisha mazingira mazuri ya biashara, kuongeza ufanisi katika utendaji kazi na kupunguza gharama na muda katika kufanya malipo.
Ameongeza kwamba Katika kutekeleza adhma ya serikali, Benki Kuu ya Tanzania imeendelea kusimamia mifumo ya malipo kwa wadau mbalimbali pamoja na kudhibiti viatarishi mbalimbali vinavyoweza kujitokeza kupitia mifumo ya malipo. Amesema Benki Kuu ya Tanzania imeweza kufanya ubunifu wa kutengeneza mfumo huo wa TIPS ambao umezingatia viwango vya kimataifa katika kutoa huduma kwa wananchi na kuwezesha ufanyaji miamala ya kifedha kwa haraka na kwa gharama nafuu zaidi.
Mkutano huo wa unafanyika tarehe 07-08 Machi 2024 kwa kauli mbiu isemayo “Kuimarisha Uwezo wa Sekta ya Fedha kuhimili misukosuko ya kiuchumi”.
Post A Comment: